Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limemkamata kijana mmoja kwa tuhuma za kuwarubuni wasichana kwa kuwapigia simu kisha kukutana nao mafichoni na kuwaingilia kimwili bila ridhaa yao na baadaye kuwapora mali walizokuwa nazo kama simu na fedha.

Kijana huyo, Paschal Sangisangi (27), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mwabului, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, anatuhumiwa kutenda makosa hayo kwa wanafunzi tofauti.

Katika taarifa iliyotolewa Juni 29, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, Juni 6, 2026, mwanafunzi mmoja (20) mkazi wa Migombani, Sengerema (jina limehifadhiwa), alipigiwa simu na mtuhumiwa na kumtongoza huku akimhadaa kuwa angempatia zawadi.

“Binti huyo alikubali kukutana na kijana huyo, ndipo alipomwingilia kimwili, kisha kumpora simu yake aina ya Samsung A42 5G yenye thamani ya Sh200,000. Kabla ya kutoweka, alimjeruhi kwa kutumia kitu chenye ncha kali sehemu ya paji la uso na kumsababishia madhara mwilini,” imesema taarifa hiyo.

Juni 10, 2026, saa 1.00 usiku, katika eneo la Soweto Mission, binti mwingine (17), mwanafunzi na mkazi wa Soweto, Sengerema, alijeruhiwa na mtuhumiwa huyo kwa kukatwa kwenye paji la uso kwa kutumia kitu chenye ncha kali, jambo lililosababisha kupata madhara mwilini.

Jeshi la Polisi limemkamata mtuhumiwa akiwa na simu yake ya mkononi aliyokuwa akiitumia kuwapigia mabinti na kuwahadaa, likiendelea kumuhoji kuhusiana na matukio hayo.

Mutafungwa amewataka mabinti na watu wengine waliofanyiwa matukio kama hayo wasione aibu kufika katika vituo vya polisi na kutoa taarifa kuhusu matukio hayo waliyotendewa na mtuhumiwa huyo au wengine katika madawati ya ukatili wa kijinsia na watoto.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya uchunguzi wa jeneza lililotelekezwa katika uwanja wa Soko la Mnada la Kabila, Kata ya Kabila, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Kamanda Mutafungwa amesema walipokea taarifa za kukutwa jeneza hilo dogo Juni 29, 2026, saa 11.00 alfajiri na kulifanyia uchunguzi.

Jeshi la Polisi limebaini kuwa jeneza hilo lilikuwa na rangi ya zambarau na msalaba wenye rangi nyeupe ambapo ndani yake vilikutwa vipande vya nyama, kichwa na miguu ya kondoo pamoja na dawa za kienyeji.

Jeshi hilo limewaomba wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu na wasiwe na imani potofu za kishirikina zinazoweza kusababisha taharuki katika jamii, au kuwashambulia kwa namna yoyote ile watu wengine kwa tuhuma za ushirikina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *