
Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, amewashauri Watanzania kuzingatia usalama wao kwa kuondoka katika maeneo yenye viashiria vya machafuko na kuelekea sehemu salama, wakati hali ya taharuki ikiendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.
Maelfu ya raia wa kigeni wanaendelea kuondoka nchini Afrika Kusini leo Jumanne, Juni 30, 2036 huku vikosi vya usalama vikitanda katika maeneo mbalimbali, hususan jimbo la KwaZulu-Natal, wakati waandamanaji wakitarajiwa kuanza maandamano kuanzia saa tano asubuhi kuelekea maeneo mbalimbali.
Taarifa iliyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini humo inaeleza hofu imetanda hasa katika jiji la Durban ambako wahamiaji wengi wameonekana katika misafara wakielekea kwenye usafiri ili kurejea katika mataifa yao.
Hata kabla ya maandamano kushuhudiwa, katikati ya jiji la Durban, makundi ya watu yameonekana yakisimamisha wanaoshukiwa kuwa wageni, kuwafanyia upekuzi na kukagua nyaraka zao za utambulisho, hali iliyoongeza hofu ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Kwa mujibu wa Watanzania waliopo Afrika Kusini, miongoni mwa watu walio katika hatari zaidi ni wale wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa Durban na sehemu nyingine za pembezoni ambako hali ya ulinzi si imara ikilinganishwa na maeneo ya mijini.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, ameeleza kuwa ubalozi unaendelea kuandaa utaratibu wa kuwasaidia Watanzania wanaotaka kurejea nyumbani, huku akisisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari.
“Kilicho muhimu kwa sasa ni kulinda maisha. Wale wanaohisi wako kwenye mazingira hatarishi ni vyema wakaangalia namna ya kwenda katika maeneo yenye usalama,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Afrika Kusini imeongeza ulinzi katika maeneo yenye hatari kubwa.
Kiongozi wa Jimbo la KwaZulu-Natal, Thami Ntuli, amesema vikosi vya usalama vimeongezwa katika maeneo mbalimbali kuhakikisha maandamano yanafanyika kwa amani na raia wote wakiwemo wageni wanalindwa dhidi ya vitendo vya vurugu.
Awali, msemaji wa Polisi wa KwaZulu-Natal, Robert Netshiunda, alinukuliwa akisema vyombo vya usalama vimejipanga kukabiliana na hali yoyote ili kuhakikisha maandamano yanafanyika kwa amani bila kuathiri waandamanaji na wageni.
Nchi nyingi tayari zimeendelea kuwasaidia raia wao kuondoka na kuwarejesha kwenye mataifa yao zikiwemo Malawi, Zimbabwe na Msumbiji, ili kupisha taharuki hiyo inayoendelea.
Wimbi hilo la hofu linafuatia matukio ya chuki dhidi ya wageni yaliyoshuhudiwa wiki za karibuni, yaliyohusisha kushambuliwa kwa wageni huku wananchi wa Afrika Kusini wanaounga mkono maandamano wakidai hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahamiaji haramu.
Serikali ya Afrika Kusini, hata hivyo, imesisitiza itahakikisha sheria inafuatwa na haitamruhusu mtu yeyote kujichukulia sheria mkononi, ikionya kuwa masuala ya uhamiaji yanasimamiwa na Serikali pekee.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.