Ripoti mpya ya UNDP iliyopewa jina Kuongezeka kwa shughuli za kijeshi Mashariki ya Kati: Kupunguza mshtuko wa kimataifa inaonesha kuwa ruzuku za mafuta duniani zinatarajiwa kufikia dola trilioni 1.1 mwaka 2026, ongezeko la dola bilioni 410 ikilinganishwa na mwaka 2025.

Katika taarifa ya UNDP kutoka New York Marekani na Hamburg Ujerumani, Afisa Msimamizi wa UNDP Alexander De Croo amesema mgogoro huo una gharama kubwa iliyojificha. “Fedha ambazo zilipaswa kujenga shule, hospitali na mifumo ya nishati safi sasa zinatumika kama ruzuku ili kunusuru uchumi usiendelee kudorora.”

Amesema hali hiyo inaweka nchi nyingi zinazoendelea kwenye wakati mgumu zaidi, hasa zile ambazo tayari zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni.

Nchi masikini na mzigo wa madeni

Kwa mujibu wa UNDP, karibu nusu ya nchi maskini duniani tayari ziko kwenye hatari kubwa ya madeni au tayari zimelemewa na madeni.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa mwaka huu nchi nyingi zinazoendelea zinatarajiwa kutumia wastani wa asilimia 9.53 ya mapato yao ya serikali kulipa riba za madeni pekee hiki ni kiwango ambacho ni mara mbili ya miaka 10 iliyopita na cha juu zaidi katika kipindi cha miaka 25.

Ripoti kwa takwimu

• Dola trilioni 1.1 – makadirio ya ruzuku za mafuta mwaka 2026
• Dola bilioni 410 – ongezeko kutoka mwaka 2025
• Dola trilioni 1.43 – ikiwa bei ya mafuta itaendelea kupanda zaidi
• Asilimia 9.53 – mapato ya serikali yatakayotumika kulipa riba ya madeni

Afisa De Croo amesisitiza kuwa suluhisho la muda mrefu ni kuongeza uwekezaji katika nishati jadidifu na kusaidia nchi zinazoendelea kupata fedha kwa urahisi zaidi. “Usalama wa nishati na mpito wa nishati safi sasa si ajenda mbili tofauti, bali ni ajenda moja.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *