
Katika kuadhimisha Siku ya siku ya Uelimishaji Kuhusu Ukatili dhidi ya Wazee Duniani (WEAAD) 2026 inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Juni, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanahimiza dunia kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu, “Zaidi ya Uelimishaji: Kufanya Kinga dhidi ya Ukatili wa Wazee Ifanye Kazi”, wakisisitiza kuwa kulinda wazee kunahitaji mifumo imara, huduma bora na ushirikiano wa karibu katika sekta mbalimbali.
Hafla maalum kuahimisha siku hii inayofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York imewakutanisha viongozi wa serikali, watetezi wa haki za binadamu na wataalamu kujadili namna jamii zinavyoweza kuzuia, kutambua na kushughulikia ukatili dhidi ya wazee kwa ufanisi zaidi.
“Ukatilii dhidi ya wazee si matokeo ya kawaida ya uzee, ni ukiukwaji wa haki za binadamu,” waandaaji wa maadhimisho hayo wamesema. “Uelimishaji ni muhimu, lakini peke yake hauwalindi watu. Tunahitaji mifumo inayofanya kazi, huduma zinazofikika na jamii zinazokataa kupuuza tatizo hili.”
Ongezeko la wazee duniani linahitaji hatua za haraka
Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati idadi ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi ikiendelea kuongezeka kwa kasi duniani.
Kati ya mwaka 2019 na 2030, idadi ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 38, kutoka watu bilioni moja hadi bilioni 1.4.
Kwa mujibuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza katika historia, wazee wanatarajiwa kuwa wengi zaidi kuliko vijana duniani, huku ongezeko kubwa zaidi likitarajiwa katika nchi zinazoendelea.
Wataalamu wanasema mabadiliko haya ya kidemografia yanahitaji umakini mkubwa zaidi katika kulinda haki, ustawi na usalama wa wazee.
“Kadiri jamii zinavyozeeka, watu wengi wenye ulemavu wanaendelea kufikia umri mkubwa, huku wazee wengi wakipata ulemavu baadaye maishani,” wameeleza wandaaji wa hafla hiyo. “Hali hii inahitaji ushirikiano mkubwa zaidi kati ya sekta zinazoshughulikia masuala ya uzee na ulemavu ili kuhakikisha hakuna mtu anayebaki bila msaada.”
Ukatili mara nyingi hufanyika kimya kimya
Licha ya kuathiri mamilioni ya watu duniani, ukatili dhidi ya wazee bado ni moja ya aina za ukatili na dhuluma ambazo hazitambuliwi wala kuripotiwa vya kutosha.
Ukatili huo unaweza kujumuisha ukatili wa kimwili, mateso ya kisaikolojia, unyonyaji wa kifedha pamoja na kutelekezwa. Mara nyingi hutokea katika mazingira ambayo wazee wametengwa, hawana msaada wa kutosha au hawafikii huduma muhimu.
“Hatari kubwa zaidi ni kutokuonekana kwa tatizo hili,” watetezi wa haki za wazee wameonya. “Wazee wanapotengwa au kupuuzwa, ukatili unaweza kuendelea bila kugundulika wala kusikika.”
Wataalamu wanaeleza kuwa kiwango halisi cha ukatili dhidi ya wazee bado hakijulikani kwa sababu waathirika wengi hushindwa au huogopa kuripoti wanachopitia.
Umoja wa Mataifa unasema takwimu zilizopo kutoka baadhi ya nchi zilizoendelea zinaonesha kuwa kati ya asilimia moja hadi kumi ya wazee hupitia aina fulani ya ukatili, lakini inaaminika kuwa idadi halisi ni kubwa zaidi.
“Takwimu zinaeleza sehemu ndogo tu ya tatizo,” wanasema watetezi wa haki za wazee. “Nyuma ya kila namba kuna mtu ambaye utu, usalama na imani yake vimevunjwa.”
Kulinda haki na utu wa wazee
Kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza kuwa kukabiliana na ukatili dhidi ya wazee kunahitaji zaidi ya kampeni za uelimishaji.
Watetezi wanataka kuwepo kwa sheria imara zaidi za ulinzi, mifumo rahisi ya kuripoti matukio, mafunzo kwa wataalamu wa afya na ustawi wa jamii, pamoja na huduma za msaada zinazoweza kutambua hatari mapema na kuchukua hatua stahiki.
“Wazee wana haki ya kuishi bila ukatili, kutelekezwa au kunyanyaswa,” wamesisitiza watetezi wa haki za wazee. “Kila hatua inayochukuliwa lazima iheshimu utu wao, uhuru wao wa kufanya maamuzi na haki zao za msingi.”
Umoja wa Mataifa pia unaeleza kuwa juhudi za kuzuia ukatili dhidi ya wazee lazima zitambue tofauti za kitamaduni na kijamii zinazoweza kuwaweka wazee katika mazingira ya hatari.
Katika baadhi ya jamii, wajane wazee hulazimishwa kuolewa tena bila ridhaa yao, huku katika maeneo mengine wanawake wazee wanaoishi peke yao wakituhumiwa uchawi na kufanyiwa ukatili au kutengwa.
Wataalam wa haki za binadamu wamesema “Suluhisho haliwezi kuwa la aina moja kwa kila jamii. Mikakati ya kuzuia unyanyasaji wa wazee lazima izingatie mazingira ya mahali husika huku ikilinda misingi ya haki za binadamu kwa wote.”
Huduma za afya na ustawi wa jamii ni muhimu
Watoa huduma za afya na maafisa wa ustawi wa jamii mara nyingi ndio watu wa kwanza wenye uwezo wa kutambua dalili za ukatili dhidi ya wazee.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa mifumo mingi bado haijajiandaa vya kutosha kugundua na kushughulikia matatizo hayo kwa wakati.
“Bila wahudumu wa afya na ustawi wa jamii kuwa na uwezo wa kutambua na kuchukua hatua haraka, visa vingi vitaendelea kufichika,” watetezi wameonya. “Wazee wengi bado wanaendelea kuteseka kimya kimya kwa sababu dalili za tatizo hazitambuliwi mapema.”
Maadhimisho ya leo ya WEAAD 2026 pia yanajadili hatua ambazo serikali na jamii zinapaswa kuchukua ili kuhakikisha juhudi za kuzuia ukatili dhidi ya wazee zinatoa matokeo halisi ya ulinzi.
Kutoka uelimishaji hadi hatua za vitendo
Wakati viongozi wa dunia wakikutana New York kujadili suala hili, ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu ni bayana “uelimishashaji lazima ufuatiwe na hatua zinazopimika.”
Watetezi wa haki za wazee wanasema kuzuia ukatili kunahitaji uwekezaji endelevu katika mifumo ya malezi na matunzo, sheria za ulinzi, elimu kwa umma na mitandao ya msaada inayowawezesha wazee kuishi kwa usalama na kujitegemea.
“Swali si tenaendepo ukatili dhidi ya wazee upo,” wanasema watetezi bali “Swali ni kama jamii ziko tayari kufanya kile kinachohitajika ili kuukomesha.”
Katika Siku hii Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa kila mtu kushiriki katika kujenga jamii inayohakikisha kila mzee anaishi kwa heshima, usalama na utu.