Serikali imekusanya jumla ya Sh1.32 trilioni hadi Juni 29, mwaka huu, ikiwa ni gawio na michango mingine kutoka mashirika na taasisi ambazo inamiliki hisa chache.
Kiwango hicho cha makusanyo ni ongezeko la Sh300 bilioni (sawa na asilimia 30), kutoka Sh1.02 trilioni kilichokusanywa Juni mwaka jana.
Kwa kipindi cha uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, mwenendo wa michango ya taasisi na mashirika ya umma umeongezeka maradufu kutoka Sh637 bilioni mwaka 2021, alipoingia hadi kufikia Sh1.32 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 108.
Hayo yameelezwa leo, Jumanne Juni 30, 2026 na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alipozungumza katika hafla ya siku ya Gawio, ambayo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni mgeni rasmi.
“Kama tungekuwa tunahesabu fedha yote inayotoka kutoka taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kiasi hiki kingekuwa kikubwa zaidi,” amesema.
Amesema mwaka huu hawakuhesabu mapato ya taasisi nne ambazo ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Sh70.7 bilioni, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Sh114.14 bilioni, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Sh208.5 bilioni, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) Sh90.39 bilioni.
Mchechu, amesema iwapo viwango vyote vya fedha vingekusanywa na kurekodiwa, jumla la gawio lingefika Sh1.811 trilioni.
(Feed generated with FetchRSS)