
Watu wengi hupata msongo wa mawazo kila mwaka wakati wa kulipa gharama muhimu kama ada za watoto, kodi ya nyumba, bima, michango ya shule au gharama nyingine zinazojirudia mara kwa mara.
Mara nyingi tunasikia watu wakisema, “Januari imefika ghafla,” au “Sijui nitatoa wapi fedha za ada.” Ukweli ni kwamba gharama hizi huwa haziji kwa kushtukiza. Tunazijua mapema na mara nyingi hutokea kwa kipindi kilekile kila mwaka. Changamoto kubwa si kutokujua gharama hizo, bali ni kutokuzipangia mapema.
Katika elimu ya fedha, gharama zinazojitokeza mara kwa mara na ambazo kiasi chake kinaweza kutabirika huitwa gharama za kudumu au (fixed obligations). Hizi ni pamoja na ada za shule, kodi ya nyumba, bima za magari au afya, marejesho ya mikopo na gharama nyingine ambazo tunajua mapema kwamba lazima zilipwe.
Tatizo kubwa linalowakumba watu wengi ni kusubiri hadi muda wa malipo ufike ndipo waanze kutafuta fedha. Matokeo yake, wengine hulazimika kukopa, kuuza mali kwa haraka au kuomba msaada kwa ndugu na marafiki. Hali hii inaweza kuepukika kwa kupanga mapema na kuweka akiba kidogokidogo kila mwezi.
Tuchukue mfano wa mzazi anayehitaji kulipa ada ya shule ya shilingi 1,200,000 kila mwezi Januari. Badala ya kusubiri Januari ifike ndipo aanze kutafuta fedha, anaweza kugawanya kiasi hicho kwa miezi 12 ya mwaka. Hii ina maana kwamba anahitaji kutenga shilingi 100,000 tu kila mwezi. Mwisho wa mwaka atakuwa amekusanya kiasi chote cha ada bila presha wala usumbufu wa kukopa.
Kanuni hii inaweza kutumika pia kwa kodi ya nyumba. Ikiwa kodi ya nyumba ni shilingi 1,800,000 kwa mwaka, badala ya kusubiri siku ya malipo ifike, unaweza kutenga shilingi 150,000 kila mwezi. Wakati wa kulipa kodi unapofika, fedha tayari zitakuwa zimekusanyika. Hii huondoa wasiwasi na kukupa amani ya akili.
Mbali na kuweka akiba, ni busara zaidi kuwekeza fedha hizo kidogokidogo katika maeneo salama yanayotoa faida ya riba au mapato mengine. Faida ya njia hii ni kwamba fedha zako zinaweza kuongezeka kupitia nguvu ya faida juu ya faida, maarufu kama (compounding). Hata kama kiasi unachoweka ni kidogo, baada ya muda kinaweza kukua na kukusaidia kufikia lengo lako kwa urahisi zaidi.
Watu wengi hukimbilia kukopa wanapokaribia kulipa gharama za kudumu. Tatizo la mkopo ni kwamba huongeza gharama nyingine za riba na ada mbalimbali. Badala ya kutumia fedha kulipa riba za mikopo, ni bora kutumia muda kupanga mapema na kujenga utaratibu wa kuweka fedha pembeni kila mwezi.
Faida nyingine ya kupanga gharama za kudumu mapema ni kuwa unapata picha halisi ya hali yako ya kifedha. Unajua kiasi gani unatakiwa kutumia leo na kiasi gani unatakiwa kuhifadhi kwa ajili ya majukumu ya kesho. Hii huongeza nidhamu ya matumizi na kukusaidia kuepuka matumizi ya papara ambayo yanaweza kuathiri malengo yako ya kifedha.
Kwa hiyo, chukua kalamu na karatasi leo. Orodhesha gharama zako zote zinazojirudia kama ada za watoto, kodi ya nyumba, bima, marejesho ya mikopo na gharama nyingine zinazojirudia.
Gawanya gharama hizo kwa miezi ya mwaka na anza kuweka fedha kidogokidogo kila mwezi. Ikiwezekana, ziweke kwenye uwekezaji salama unaokuwezesha kupata faida kidogo. Utakapofika muda wa kulipa, hutakuwa na wasiwasi, hutahitaji kukopa, na utakuwa umejenga tabia muhimu ya uhuru wa kifedha.
Kumbuka, gharama nyingi za kudumu haziji kwa kushtukiza. Tunazijua mapema. Hekima si kusubiri mpaka zifike, bali ni kujiandaa mapema. Maandalizi ya leo ndiyo amani ya kesho.