
Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda amesema idadi ya walipakodi wa nchini imefika milioni 8.4 na jitihadi zinaendelea ili kupata walipakodi wengi zaidi.
Mwenda anasema hayo wakati mamlaka hiyo ikiadhimisha miaka 30 tangu ianze kutoa huduma nchini. TRA iliundwa na Serikali ya awamu ya pili chini ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi lakini ilianza kufanya kazi Julai Mosi mwaka 1996.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka hiyo yaliyofanyika jana, Mwenda alisema miaka 30 iliyopita jumla ya walipakodi nchini walikuwa 75,000 lakini sasa idadi yao imeongezeka mara dufu.
“Kwa sasa walipakodi nchini wapo milioni 8.4 hao wanajumuisha wafanyakazi, wafanyabiashara wakubwa wa kati na wadogo. Tunaendelea na kupanua wigo wa walipakodi kwani kundi la watu wenye uwezo wa kuzalisha mali nchini lina watu zaidi ya milioni 34,” alisema Mwenda.
Kuhusu makusanyo Mwenda alisema kwa mara ya kwanza mamlaka hiyo inakwenda kuweka rekodi ya wastani wa makusanyo ya Sh3trilioni kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia juzi Juni 30, 2026 akisema siri ya mafanikio ni pamoja na matumizi ya Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) na Mashine za risiti za EFD.
Mwenda aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 30 ya uwepo wa TRA njia za kidijitali za ukwepaji kodi zimekuwa zikitafutwa na kupitia mfumo mpya wa usimamizi wa kodi za ndani IDRAS TRA itaweza kufuatilia walipakodi wote kwa kushirikiana na taasisi nyingine ambazo mifumo yake inasomana na mifumo ya TRA.
Anasema kabla ya Julai mosi, 1996 mamlaka hiyo ilikuwa ikikusanya Sh24 bilioni kwa mwezi na kiwango hicho kimekuwa kikiongeze kila mwaka kutokana na ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa walipakodi na kuongezeka kwa mbinu za ukusanyaji na udhibiti wa upotevu wa mapato.
Katika mkutano huo aliwashukuru walipakodi wote kwa mchango wao huku akisema matumizi ya teknolojia yanakwenda kuongeza makusanyo ya taasisi hiyo pamoja na kuongeza weledi sanjari kudhibiti mianya ya rushwa.
Ili kuongeza mapato zaidi Mwenda alitoa rai kwa wananchi wote kushiriki katika kuwafichua wakwepa kodi ili kuisaidia kuongeza makusanyo ya nchi huku akibainisha kuwa TRA huwalipa wale wote wanaosaidia kutoa taarifa hizo.
Pamoja na kuwalipa Mwenda alisema Mamlaka hiyo ina utaratibu thabiti za kuwalinda watoa taarifa za uvujaji wa mapato hivyo mtoa taarifa hapaswi kuwa na wasiwasi wowote.
Mwenda alisema vitendo vya ukwepaji wa kodi vimekuwa vikidhoofisha uchumi wa nchi na kuondoa ushindani sokoni hivyo wananchi wanaoshiriki kuwafichua wakwepa kodi watakuwa wameisaidia nchi.
Anasema kwa miaka 30 TRA imefanikiwa kuwa karibu zaidi na walipakodi hali ambayo imeongeza ulipaji kodi kwa hiari na imani ya walipakodi kwa TRA na hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa kwa makusanyo ya kodi zinazokwenda kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.