Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuijenga Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa juu unaoongozwa na viwanda, teknolojia, ubunifu na ushindani wa kimataifa.

Hata hivyo ili kufikia malengo hayo nchi inahitaji rasilimali za kutosha lakini pia kutahitajika taasisi imara zenye uwezo wa kushindana katika soko la dunia.

Kwa miaka mingi, baadhi ya mashirika ya umma yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za gharama kubwa za uendeshaji, utegemezi wa Serikali na mifumo isiyoendana na kasi ya ushindani wa dunia ya sasa.

Wakati Dira 2050 inapoanza kutekelezwa, Serikali Juni 30, mwaka huu, ilitangaza uamuzi mgumu unaolenga kuzifanya taasisi na mashirika ya umma kuwa na nguvu ya ushindani katika soko la dunia na uwezo wa kujitegemea.

Katika hotuba yake ya Siku ya Gawio, Rais Samia Suluhu Hassan alisema, “Utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji taasisi zenye uwezo wa kuingia kwenye ushindani wa soko. Tunapoanza kesho (Julai 1) utekelezaji wa dira tunatakiwa kuwa makini kwelikweli, taasisi zetu ziwe imara kwelikweli.”

Kwa taasisi zinazosuasua, alisema zitafutiwe tiba ili kwenda nazo sambamba katika utekelezaji wa dira hiyo, akisisitiza zitahitajika taasisi zinazotumia teknolojia, zinazopunguza upotevu wa mali, kuvutia mitaji na kufungua fursa kwa sekta binafsi.

Msisitizo wa hoja yake ni kile alichosema, umakini unahitajika kwenye uongozi na usimamizi katika kuendesha mashirika na taasisi za umma.

“Dira ya 2050 haitakamilika kwa mipango na utajiri wa rasilimali, bali itatekelezwa kwa namna rasilimali hizo zitakavyosimamiwa, kulindwa na kugeuzwa kuwa fursa, huduma na maendeleo kwa wananchi,” alisema.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Maryland nchini Marekani, Dk Joseph Werema, anasema maelekezo hayo ya Rais yanagusa moja ya changamoto zinazokwamisha mashirika mengi ya umma Afrika, kushindwa kushindana katika soko huria.

Anasema shirika lenye ushindani si lazima liwe kubwa kwa wingi wa mali au idadi ya wafanyakazi, bali liwe na uwezo wa kutoa huduma au bidhaa kwa ubora, gharama nafuu na kwa kasi inayolingana na viwango vya kimataifa.

“Leo dunia inashindana kwa tija. Kama shirika linatumia siku 20 kufanya kazi ambayo mshindani wake anaifanya kwa siku mbili, tayari limepoteza ushindani. Kama linatumia wafanyakazi wengi kuzalisha matokeo madogo, tayari lina tatizo,” anaeleza.

Dk Werema, anaeleza ili mashirika ya Tanzania yafikie kiwango hicho, ni lazima yawekeze katika teknolojia, mifumo ya kidijitali na kuongeza ujuzi wa watumishi.

Tatizo lililopo sasa katika baadhi ya mashirika, anasema ni gharama kubwa za uendeshaji, mifumo ya zamani ya kazi, ucheleweshaji wa maamuzi na utegemezi mkubwa kwa Serikali.

“Baadhi ya mashirika bado yanafanya kazi kana kwamba yapo katika uchumi wa miaka ya 1980 wakati dunia imeingia katika uchumi wa akili unde, data na ubunifu. Huko ndiko kunakopunguza uwezo wa kushindana,” anasema.

Mchambuzi wa Uchumi, Dk Beneth Aloyce, anasema maelekezo ya Rais ni kuandaa taasisi zitakazoweza kuhimili ushindani wa kikanda na kimataifa katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

Anasema Dira 2050 inalenga uchumi mkubwa zaidi, wenye viwanda vingi zaidi, biashara kubwa zaidi na uwekezaji mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.

“Huwezi kufika huko ukiwa na mashirika yanayoshindwa hata kushindana ndani ya soko la Afrika Mashariki. Lazima yawe na uwezo wa kuvutia wawekezaji, kushirikiana na kampuni za kimataifa na kuingia katika minyororo ya thamani ya dunia,” anasema.

Anafafanua kuwa, mashirika yenye ushindani hujenga imani kwa wawekezaji kwa sababu yana mifumo mizuri ya utawala, uwazi katika matumizi ya fedha na uwezo wa kutoa matokeo yanayopimika.

Kwa mtazamo wake, changamoto iliyopo sasa si uhaba wa rasilimali pekee, bali ni ufanisi wa kuzitumia rasilimali hizo.

“Tanzania ina rasilimali nyingi sana. Tunayo gesi, madini, ardhi, bandari na soko kubwa. Lakini rasilimali hizo zitakuwa na thamani pale tu taasisi zinazozisimamia zitakuwa na uwezo wa kuzigeuza kuwa faida za kiuchumi,” anasema.

Dk Aloyce, anasema dunia ya mwaka 2050 itakuwa tofauti kabisa na ya sasa. Ushindani hautakuwa kati ya nchi na nchi pekee, bali kati ya taasisi, kampuni na mifumo ya uzalishaji.

Katika mazingira hayo, anasema mashirika ya Tanzania yatatakiwa kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kushiriki katika biashara za kikanda na kimataifa na kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.

Pia, anasema ni muhimu yatengeneze ajira zenye tija kwa vijana, yachangie mapato ya Serikali kupitia kodi na gawio na yalete teknolojia na ubunifu mpya katika uchumi.

Anasisitiza bila mashirika yenye ushindani, utekelezaji wa Dira 2050 unaweza kukwama kwa sababu Serikali italazimika kutumia muda mwingi kuyaokoa mashirika yanayopata hasara badala ya kuelekeza nguvu katika uwekezaji wa maendeleo.

“Ndiyo maana kauli ya Rais Samia inaweza kutafsiriwa kama wito wa mageuzi ya taasisi za umma yanayolenga kuzifanya ziondoke katika utegemezi wa Serikali na kuingia katika zama za ushindani, tija, teknolojia na uwajibikaji.

“Huo ndio msingi utakaoibeba Tanzania kuelekea uchumi mkubwa na shindani unaolengwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” anasisitiza.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutegano Mwinuka, anasema vitu vingi vimeshaanza kufanyika kuhakikisha taasisi zinafuata mwelekeo huo.

Anasema kila taasisi au shirika la umma, lina mipango mikakati ya miaka mitano iliyoandaliwa kwa kuzingatia malengo ya dira ya taifa.

“Ushindani una maana kubwa kwa sababu ndiko kunapatikana ufanisi, ufanyaji kazi wa tija na mwisho wa siku, huduma zinatolewa vizuri kwa kasi inayoendana katika kutekeleza dira,” anasema.

Mambo ya kuzingatia

Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa zamani wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benedict Mongula, anasema muhimu ni kuwa na taasisi zitakazokuwa na uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi na matokeo yanayoonekana.

Anasema kauli ya Rais Samia imegusa eneo nyeti ambalo kwa muda mrefu limekuwa changamoto kwa mashirika mengi ya umma, uwezo mdogo wa kitaasisi unaosababisha baadhi yao kushindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya uchumi wa dunia.

“Kama tunataka mashirika yetu yawe na ushindani wa kweli, lazima tuanze kwa kujenga uwezo wa ndani wa taasisi hizo. Ushindani hauanzi kwenye majengo mazuri, unaanzia kwenye watu wenye ujuzi, mifumo imara na usimamizi bora,” anasema

Profesa Mongula, anasema hatua ya kwanza ni kuimarisha rasilimali watu kwa kuhakikisha taasisi zinakuwa na wataalamu wa kutosha katika maeneo muhimu ya sheria, fedha, uhasibu, uhandisi, teknolojia na usimamizi wa biashara.

Kwa mujibu wake, uchumi wa kisasa unahitaji taasisi zinazoweza kufanya uamuzi sahihi kwa wakati, kutambua hatari mapema na kutumia fursa zinazojitokeza katika soko la ndani na la kimataifa.

“Taasisi yenye wataalamu wa kiwango cha juu ina uwezo mkubwa wa kuvutia uwekezaji, kupunguza makosa ya kiutendaji na kuongeza tija katika utoaji wa huduma au uzalishaji,” anasema.

Anasema pamoja na utaalamu, suala la usimamizi linapaswa kupewa uzito mkubwa zaidi. Kwa maoni yake, taasisi nyingi zinazosuasua hazikosi fedha au rasilimali, bali zinakabiliwa na mifumo dhaifu ya usimamizi na uwajibikaji.

Anaeleza kuwa bodi za wakurugenzi zinapaswa kuwa na watu wenye uwezo, uzoefu na maono ya kimkakati ili ziweze kutoa mwelekeo sahihi wa taasisi na kusimamia matumizi ya rasilimali kwa tija.

“Taasisi inaweza kuwa na wataalamu wazuri na fedha za kutosha, lakini ikiwa usimamizi wake ni dhaifu, matokeo yatakuwa hafifu. Uongozi bora ndiyo injini ya mafanikio ya taasisi yoyote,” anasema.

Profesa Mongula, anasisitiza umuhimu wa kuimarisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama), akisema ushindani wa karne ya sasa unaamuliwa zaidi na uwezo wa taasisi kutumia taarifa na teknolojia katika kufanya maamuzi.

Anasema taasisi zinapaswa kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kuhifadhi, kuchambua na kusimamia taarifa ili kuongeza ufanisi, kupunguza upotevu wa rasilimali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na wawekezaji.

“Katika uchumi wa sasa, taarifa ni mtaji. Taasisi isiyojua kukusanya, kuhifadhi na kutumia taarifa kwa usahihi itakuwa na wakati mgumu kushindana na taasisi za kisasa duniani,” anaeleza.

Aidha, anasema ni muhimu kuweka mifumo bora ya motisha kwa wafanyakazi ili kuongeza ari ya kazi na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi wanazozihudumia.

Kwa mtazamo wake, wafanyakazi wenye ujuzi na wanaotambua mchango wao unathaminiwa huwa wabunifu zaidi, waadilifu zaidi na wenye uwezo mkubwa wa kusukuma taasisi kufikia malengo yake ya kimkakati.

“Tukijenga uwezo wa kitaalamu, tukaimarisha usimamizi, tukatumia teknolojia kwa ufanisi na kuweka motisha stahiki kwa watumishi, tutakuwa tumeweka msingi imara wa mashirika yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa katika utekelezaji wa Dira 2050,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *