
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Sera, Mahusiano ya Serikali na Ushirikiano kwa Afrika wa Gates Foundation, Caty Fall Sow, yakilenga kuimarisha ushirikiano katika kuboresha afya ya mama na mtoto nchini Tanzania na barani Afrika.
Mazungumzo hayo, yaliyofanyika leo Alhamisi Julai 2, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam, yamekuja wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto, huku Rais Samia akiwa ameteuliwa kuwa Bingwa wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Mama, Mtoto Mchanga na Mtoto.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, pande hizo mbili zilijadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Gates Foundation katika maeneo mbalimbali ya afya ikiwemo ya mama na mtoto, chanjo, lishe, kuimarisha mifumo ya huduma na kudhibiti magonjwa.
Katika mazungumzo hayo, Caty Fall Sow amempongeza Rais Samia kwa kuteuliwa kuwa Bingwa wa Umoja wa Afrika katika afya ya mama na mtoto, akieleza kuwa nafasi hiyo ni muhimu katika kuhamasisha nchi za Afrika kuongeza juhudi za kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya kina mama na watoto.
Aidha, amesema Gates Foundation itaendelea kushirikiana na Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na Waafrika wenyewe katika kuboresha huduma za afya kwa wanawake na watoto.
Taasisi hiyo pia ilieleza kuridhishwa na hatua ambazo Tanzania imezipiga katika kupanua miundombinu ya afya, kuimarisha huduma ya msingi, kuboresha huduma za mama wajawazito na watoto wachanga pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu zinazookoa maisha.
Kwa upande wake, Rais Samia amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, za dharura kwa wajawazito, za watoto wachanga na programu za chanjo, hatua ambazo zimechangia kuboresha matokeo ya afya ya mama na mtoto nchini.
Rais Samia pia ameeleza maandalizi yanayoendelea ya kuandaa ramani ya pamoja ya Bara la Afrika chini ya jukumu lake kama Bingwa wa AU.
Ramani hiyo inalenga kuhamasisha viongozi wa kisiasa kuongeza uwajibikaji, kuimarisha uwekezaji katika sekta ya afya na kuharakisha utekelezaji wa mikakati ya kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika vya kina mama, watoto wachanga na watoto barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pande zote mbili zilisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kudumu unaojengwa katika ubunifu, uwekezaji na suluhisho zinazoongozwa na nchi za Afrika ili kuboresha afya na ustawi wa wanawake na watoto katika bara zima.
Mazungumzo hayo yanaongeza msukumo wa juhudi za Tanzania za kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya afya, huku yakitoa nafasi ya kuongeza rasilimali na utaalamu unaohitajika kufikia malengo ya kupunguza vifo vya kina mama na watoto na kuboresha huduma za afya kwa vizazi vya sasa na vijavyo.