MSHAMBULIAJI Prince Dube, amepiga chini ofa tatu na kufanya uamuzi mgumu wa kurejea kwao Zimbabwe akisaini mkataba wa miaka miwili timu iliyopanda daraja kushiriki Ligi Kuu nchini humo.

Dube amesaini mkataba huo na Hardrock ya kwao Zimbabwe baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga mwisho wa msimu huu 2025-2026.

Awali Yanga ilimuwekea mshambuliaji huyo ofa mezani ya kuongeza mkataba, akakubali lakini baadaye akabadili mawazo akitaka kutafakari upya.

Leo Julai 2, 2026, Hardrock inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Zimbabwe, imemtambulisha mshambuliaji huyo kuwa mchezaji wao mpya baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika.

Kabla ya kukubali kutua Hardrock, Dube alipokea ofa ya Sh1 bilioni kusaini Al Ittihad ya Libya lakini mshambuliaji huyo akaigomea.

Ofa nyingine kubwa ni ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo ilitaka kumpa kiasi cha Sh950 milioni lakini nayo akaigomea, huku ikiwa bado haijafahamika Hardrock imempa kiasi gani katika dili hilo na kukubali.

Dube msimu huu 2025-2026 amefanikiwa kumaliza kwa kuifungia Yanga mabao 10 katika Ligi Kuu ya NBC akizidiwa manne na kiungo Allan Okello aliyekuwa kinara ndani ya timu hiyo. Huku kinara wa jumla ni Mosi Nduwumwe wa Singida Black Stars aliyefunga mabao 17.

Mzimbabwe huyo ameachana na Yanga baada ya kuitumikia kwa misimu miwili akitua 2024-2025 akitokea Azam.

Kwa sasa Hardrock inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Zimbabwe inayoendelea baada ya kucheza mechi 19 ikikusanya pointi 38, ikizidiwa tano na kinara Scottland FC yenye 43 ikicheza mechi 20.

Ligi Kuu ya Zimbabwe inashirikisha timu 18, hivyo Hardrock yenye maskani yake Kwekwe ikiwa imepanda daraja msimu huu, imebakiwa na mechi 15 kuhitimisha msimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *