
Arusha. Haijaisha mpaka imalizike, ndio usemi unaweza kuutumia kuelezea namna Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Yahaya Mokiwa, anavyoruka viunzi vya mapingamizi mahakamani, katika harakati zake za kupinga kushushwa cheo na mwajiri wake.
Mwaka 2025, Mokiwa ambaye anapinga kushushwa cheo kutoka Mkaguzi wa Polisi (Inspector) hadi Mkaguzi Msaidizi, alifungua maombi namba 32706 akiomba kupatiwa kibali cha mahakama, ili afungue maombi ya mapitio ya mahakama.
Ofisa huyo alieleza kuwa alishushwa cheo kwa madai ya tuhuma za kinidhamu Januari 7,2025, akakata rufaa Februari 2025 lakini rufaa yake haikusikilizwa lakini adhabu aliyopewa ilithibitishwa kwa barua ya Julai 30, 2025 bila sababu zozote.
Wajibu maombi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Tume ya Utumishi ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji, na Uhamiaji, Katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), waliwasilisha pingamizi.
Hata hivyo, Machi 9, 2026 Jaji, Frank Mahimbali wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha alitupilia mbali pingamizi hilo akisema alichokieleza Mokiwa kinaleta maswali mazito ya uhalali, taratibu na kushindwa kutekeleza wajibu wa kisheria.
Jaji Mahimbali alisema pingamizi hilo la awali limetupiliwa mbali kwa kukosa sifa na kasoro ya kiutaratibu na kwamba mwombaji ameonyesha ana kesi inayofaa kwa mapitio ya mahakama hivyo mahakama inamruhusu kufungua shauri hilo.
Alivyoruka kiunzi cha pili
Baada ya kuruhusiwa kufungua maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review) kupinga uamuzi wa kumshusha cheo, Ofisa huyo akafungua maombi namba 7334 ya 2026 dhidi ya wajibu maombi wal wale wanne, akiwamo IGP na AG.
Kama ilivyokuwa wakati wa maombi ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, safari hii tena wajibu maombi hao wanne wakawasilisha pingamizi la awali likiwa na hoja mbili, wakitaka maombi hayo yatupiliwe mbali na mahakama.
Hoja za pingamizi ni kwamba maombi ni mabaya kisheria kwa kuwa na taarifa ambayo haikuwa kwenye maombi ya kibali na pili upelekaji wa nyaraka za maombi haya imepitwa na wakati kinyume na Kanuni zinazosimamia mashauri hayo.
Wakili wa Serikali, Joseph Bundala alisisitiza kuwa maombi hayo ya mapitio ya mahakama hawakuyapata (served) ndani ya siku saba kama sheria inavyotaka, hoja ambazo zilipanguliwa na wakili wa mleta maombi, Efrahim Kisanga.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kisanga alisema pingamizi la wajibu maombi mwombaji aliwasilisha kuwa wajibu maombi limedhaniwa vibaya (misconceved), lisilo na sifa, na linapaswa kutupiliwa mbali na wajibu maombi waamriwe kulipa gharama.
Wakili huyo alisema wakati mwombaji anazuiwa kuanzisha sababu mpya baada ya kibali kutolewa, sheria haizuii ufafanuzi au uainishaji wa ukweli wa masuala ambayo tayari yalishaelezwa katika hoja za maombi ya kupatiwa kibali.
Kwa mujibu wa wakili, alisema hoja yake kuu ni kwamba maombi yalibaki yakiwa yameimarishwa kwa misingi ileile ambayo ruhusa ilitolewa, yaani uharamu, upotovu wa taratibu, uvunjaji wa haki ya asili na kutekeleza wajibu wa kisheria.
Mwombaji aliendelea kudai kuwa wajibu maombi walishindwa kubainisha kwa uwazi madai ya misingi mipya au taarifa mpya zinazosemekana kuwa zimeletwa katika msingi maombi na kukosekana kwa maelezo kama hayo, Mahakama haiwezi kuamua ipasavyo kama Kanuni ya 8(1)(a) imekiukwa.
Aliendelea kujenga hoja kuwa hata kama kuna nyongeza ya jambo limeanzishwa, dawa ifaayo huyatupilia mbali maombi na badala yake kujikita katika shauri kwa misingi ambayo kibali cha kufungua maombi ya mapitio kilikuwa kimetolewa.
Kuhusu hoja ya pili ya pingamizi kwamba wajibu maombi walipewa taarifa na nyaraka nje ya muda wa siku saba, wakili Kisanga haikujumuisha pingamizi sahihi la awali kwa sababu uamuzi wake ulitegemea mambo ya kweli yanayobishaniwa.
Mwombaji pia alieleza kuwa walalamiwa hawakutoa ushahidi wowote wa kuunga mkono madai yao kwamba huduma ilitekelezwa nje ya muda uliowekwa.
Uamuzi wa Jaji
Jaji katika uamuzi wake alisema baada ya kupitia mabishano ya hoja za kisheria, alisema kuamua kama maombi hayo yana dosari kisheria kwa kuwapatia upande wa pili nje ya muda, kuna haja ya kupima kama pingamizi ni halali.
Akirejea msimamo wa sheria, Jaji alisema pingamizi la awali lina hoja safi ya sheria ambayo yakizingatiwa, inaweza kuondoa shauri bila ya ulazima wa kuita ushahidi.
“Mahakama zaidi ilitahadharisha kuwa pingamizi la awali haliwezi kujengwa juu ya ukweli au mambo yanayobishaniwa inayohitaji uchunguzi wa ukweli,”alisema Jaji.
“Wajibu maombi waliwasilisha kuwa mwombaji alianzisha taarifa na mambo mapya katika maombi, ambayo hayakuwamo katika taarifa inayoambatana na maombi ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama.”
“Mwombaji, kwa upande mwingine, alisema kuwa muhimu maombi yamefafanuliwa tu na mambo maalumu ambayo tayari yamefichuliwa wakati wa maombi ya kibali na hakuna msingi mpya ulioanzishwa,” alisema Jaji.
“Halikadhalika muombaji ameeleza kuwa wajibu maombi wameshindwa kubainisha taarifa maalumu zinazodaiwa kutoendana na maombi ya kibali.”
“Ninaona hoja ya mwombaji ina mashiko. Ikiwa kuna tofauti ya nyenzo kati ya taarifa iliyowasilishwa hatua ya kibali na taarifa inayoambatana na hoja kuu maombi yanaweza kuanzishwa tu baada ya kulinganisha hati mbili.”
“Kwa hivyo naona kwamba hoja ya kwanza ya pingamizi haitoi hoja safi ya sheria hivyo haiwezi kusimama kama pingamizi la awali,”alisema.
“Kuhusu pingamizi la pili, Kanuni ya 9(1) ya Kanuni za Mapitio ya Mahakama ya inataka mwombaji kutuma maombi ya msingi na nyaraka za usaidizi ndani ya siku saba baada ya kufungua, lakini kuna tatizo katika msingi wa pingamizi lao.”
“Uamuzi wa kama huduma ilitekelezwa nje ya muda wa siku saba uliowekwa inahitaji Mahakama kuhakikisha tarehe ya kufungua, tarehe ya kuandikishwa, tarehe ambayo hati zilipatikana kwa huduma, na tarehe halisi ya huduma.”
“Katika uchambuzi wa mwisho, naona kwamba hoja zote mbili za pingamizi la awali zinahitaji ukweli na uhakikisho kabla ya kubainishwa. Ni kwa msingi huo pingamizi hilo linakataliwa na maombi yataenda hatua ya usikilizwaji kamili,” alisema.