
Iran imetoa onyo kwa nchi za kikanda kuwa zichukue tahadhari ya juu dhidi ya mipango ya usalama inayoongozwa na Marekani, ikisema kuwa nchi hizo zisizahau athari za uvamizi wa kijeshi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel uliovuruga usalama katika ukanda mzima wa Asia Magharibi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amekosoa dhana ya ulinzi unaodaiwa kuongozwa na Marekani, akisema kuwa vikosi vya Marekani havijatuletea chochote ila fujo na ukosefu wa utulivu katika ukanda wa Asia Magharibi.
Akijibu moja kwa moja tangazo la Kamandi ya Jeshi la Marekani, CENTCOM , kuhusu mazungumzo ya kijeshi yanayofanyika nchini Bahrain kwa kushirikisha maafisa kutoka nchi mbalimbali za kikanda, Araghchi ameuliza hivi kupitia mtandao wa X usiku wa Alhamisi, “Je, CENTCOM imeleta usalama au ukosefu wa usalama katika ukanda wetu?”
“Jibu liko wazi,” alisema.
Araghchi ameendelea kusisitiza nguvu ya kijeshi ya Iran isiyo na kifani: “Vilevile, Majeshi yetu yenye nguvu yamedhinisha kuwa wageni hawawezi hata kujilinda wenyewe. Amani katika ukanda wetu inaweza kudumishwa tu ikiwa itakuwa jumuishi na pana, bila kuingiliwa na nguvu za nje.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, naye amelaani Marekani kuhusiana na mkutano huo wa usalama wa kikanda unaofanyika Bahrain, akiwaonya majirani wasidanganywe na mipango ya usalama ya Washington na wawe macho dhidi ya mchango wake wa kuvuruga utulivu katika Asia Magharibi.
“Utawala wa Marekani umeonyesha mara kwa mara kuwa hauthamini amani na usalama wa nchi za ukanda wa Asia Magharibi.”
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa X amesema:
“Mikusanyiko kama hiyo si kitu kingine ila ni igizo na jitihada za uhusiano wa umma (PR) zenye lengo la kufunika sera za Marekani za kuvuruga utulivu na vitendo vya kinyume cha sheria katika Asia Magharibi.”
Akijibu taarifa ya Marekani iliyotangaza mkutano huo wa Bahrain kuwa eti ni “Mazungumzo ya Usalama wa Kikanda”, amesema: “Nchi za ukanda huu lazima ziendelee kuwa macho na kuwa waangalifu sana, na hazipaswi kusahau masomo ya wazi ya athari za uvamizi wa kijeshi wa hivi karibuni wa Marekani na utawala wa Kizayuni pamoja na vitendo vyao vya uharibifu vilivyovuruga usalama wa ukanda mzima.”
Usiku wa Jumatano, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilitangaza kuwa imefanya mkutano wa usalama wa kikanda ulioratibiwa na Jeshi la Bahrain, ukihudhuriwa na maafisa wakuu wa kijeshi kutoka nchi 11 za Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).
Kwa mujibu wa taarifa ya CENTCOM, Kamanda Jenerali Brad Cooper pamoja na maafisa wakuu wa kijeshi kutoka Bahrain, Misri, Jordan, Kuwait, Lebanon, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Falme za Arab Mashariki, na Yemen, walijadili hali ya sasa ya usalama katika ukanda huo na fursa za kuimarisha ushirikiano wa kijeshi.
Washiriki pia walisisitiza azma yao ya pamoja ya kuhakikisha upitishaji huru wa biashara kupitia Bahari ya Hormuz (Strait of Hormuz).
Onyo hilo la Iran linakuja wiki chache baada ya vita vya uvamizi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Katika kujibu uchokozi huo, majeshi ya Iran yalifanya mashambulizi makali ya kulipiza kisasi katjeshi la Marekani vilivyo katika nchi za eneo.
Aidha wakati wa vita Iran iliweka vikwazo vya usafiri katika Lango Bahari la Hormuz, kabla ya usitishaji wa vita na makubaliano ya awali (MoU) kati ya Iran na Marekani kufanya hali ya utulivu kurejea kwa kiasi fulani.