
Leo ni Ijumaa tarehe 18 Muharram 1448 Hijria sawa na Julai 3 mwaka 2026.
Siku kama ya leo, miaka 155 iliyopita alizaliwa Allamah Haidar Quli Sardar Kabuli, alimu mkubwa na mtaalamu wa fiqhi mjini Kabul, Afghanistan.
Akiwa kijana mdogo Allamah Sardar Kabuli alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa enzi hizo kama vile, Mirza Hussein Nuri na Sayyid Swafiyyud-Din Hassan bin Hadi Kadhimi, sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwa maulama na maraajii watajika kama vile, Sayyid Hassan Sadr naHaji Sheikh Abbas Qumi, ambapo pia alipata ijaza (idhini) ya kunakili na kuandika riwaya na hadithi.
Mwaka 1310 Hijiria, Allamah Haidar Quli Sardar Kabuli alielekea mjini Kermanshah, Iran na kujishughulisha na ufundishaji kwa wakazi wa mji huo sanjari na kuandika vitabu kadhaa. Msomi huyo alisomea lugha kadhaa za dunia, kama vile Kiarabu, Kingereza, Kiebrania na Urdu. Kitabu cha ‘Tarjama ya Injili ya Barnaba’ na ‘Hadithi 40 katika fadhila za Amirul-Muuminin’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo.
Allamah Haidar Quli Sardar Kabuli alifariki dunia mwaka 1372 Hijiria, akiwa na umri wa miaka 79 na kuzikwa mjini Najaf, Iraq. ***
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia.
Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’.
Hadi mwisho wa uhai wake msomi huyo alisalia mjini Tehran na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum. *****
Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita inayosadifiana na 3 Julai 1904, alifariki dunia Theodor Herzl, mwasisi wa harakati ya kimataifa ya Kizayuni.
Herzl alizaliwa mwaka 1860 huko Bucharest mji mkuu wa Hungary na kisha kuelekea Austria. Mnamo mwaka 1897 aliunda Taasisi ya Kimataifa ya Kizayuni kwenye kongamano lililofanyika nchini Uswisi.
Herzl alibuni mikakati ya kuasisiwa utawala ghasibu na wa Kizayuni wa Israel kwenye ardhi za Palestina, utawala ambao hadi leo unaendelea kufanya jinai kubwa na kusababisha maafa yasiyo na kifani dhidi ya raia madhlumu wa Palestina. ***
Tarehe 12 Tir 1349 Hijria Shamsia, yaani siku kama ya leo miaka 56 iliyopita alifariki dunia Allamah Abdul Hussein Amini, faqihi mkubwa na mwandishi hodari na mashuhuri wa Kiislamu.
Kitabu cha kwanza cha mwanazuoni huo alikipa jina la Shuhadaul Fadhila. Hata hivyo kitabu mashuhuri na kikubwa zaidi cha Allamah Amini ni kile cha “al Ghadiir Fil Kitabi Wassunah”. Ndani ya kitabu hicho Allama Amini amekosoa na kuchunguza vitabu vikubwa na marejeo vya Kiislamu 150 akithibitisha wilaya na haki ya Imam Ali bin Abi Twalib ya kuwa Khalifa na Imam wa Waislamu baada tu ya Mtume Muhammad (saw).
Mwanazuoni huyo alisafiri kwa taabu katika nchi nyingi kama India, Uturuki, Syria, Misri na Iraq kwa ajili ya kukusanya ushahidi mbalimbali wa kihistoria alioutumia katika kitabu hicho. *****
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita ndege ya abiria aina ya Airbus ya Shirika la Ndege la Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas, kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi.
Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama wa serikali ya Marekani.
Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa. ***
Na Tarehe 3 Julai miaka 13 iliyopita rais wa zamani wa Misri kutoka harakati ya Ikhwanul Muslimin, Muhammad Morsi aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na jeshi la nchi hiyo.
Mapinduzi hayo yaliongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Sisi. Morsi alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Misri baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011. Hata hivyo mwanasiasa huyo hakuweza kutatua matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya muda mrefu ya nchi hiyo. Vilevile licha ya kwamba alihesabiwa kuwa katika safu za wanaharakati wa Kiislamu lakini alidumisha uhusiano wa karibu na utawala haramu wa Israel na akatangaza kutambua rasmi mkataba ya Camp David na utawala huo haramu.
Muhammad Morsi alitekeleza siasa zisizo sahihi kuhusu baadhi ya nchi za Kiislamu na hatimaye akasalitiwa na nchi alizozitegemea ambazo ziliwaunga mkono na kuwasaidia wale waliomuondoa madarakani. ****