Makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina yamesisitiza kuhusu “haki ya Wapalestina kupinga uvamizi kwa namna yoyote ile” na kukataa “usimamizi wowote wa kigeni” katika mambo ya ndani ya Palestina, wakati Gaza ikifikisha siku ya 1,000 ya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala katili Israel ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina wasipungua 73,000.

Taarifa ya pamoja ya makundi ya Palestina iliyotolewa Alhamisi imesema: “Siku elfu moja zimepita tangu kuanza kwa mauaji ya kimbari ya Wazayuni huko Gaza, yakitekelezwa kwa msaada wa moja kwa moja kutoka kwa utawala wa Marekani na serikali za nchi za Magharibi.”

Vikundi hivyo vilitangaza kuwa Israel imeshindwa kufikia malengo yake haramu ya kivita, ikiwemo kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao ya jadi huko Gaza licha ya uharibifu mkubwa na janga la kibinadamu.

Harakati hizo za kupigania ukombozi wa Palestina zimesisitiza “umuhimu wa kuongeza kasi ya muqawama au mapambano katika Ukingo wa Magharibi, al-Quds (Jerusalem), na ardhi yetu yote inayokaliwa kwa mabavu” na kusisitiza kuwa utawala wa Gaza ni “jambo la ndani kabisa la Wapalestina.”

Taarifa hiyo inatolewa huku Israel ikiendelea kukiuka makubaliano ya usitishaji vita yaliyoungwa mkono na Marekani yaliyoanza mwezi Oktoba. Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza, majeshi ya Israel yamefanya mamia ya ukiukaji tangu kusitishwa kwa mapigano kuanze, na kuua zaidi ya Wapalestina 1,000 na kujeruhi wengine 3,406.

Siku ya Jumatano pekee, majeshi ya Israel yalifanya ukiukaji 17 wa usitishaji vita, na kusababisha vifo vya Wapalestina wanne.

Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza ilitoa ripoti kamili ya takwimu ikiadhimisha siku ya 1,000 ya mauaji ya kimbari yaliyoanza Oktoba 7 2023, ikifichua kuwa Wapalestina 73,066 wamethibitishwa kuuawa shahidi, wakiwemo watoto zaidi ya 21,500 na wanawake 12,500, huku watu 9,500 wakiwa bado hawajulikani walipo, wakiwemo wale walio chini ya vifusi au ambao hatma yao haijulikani.

Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa Wapalestina 173,514 wamejeruhiwa, huku 5,400 wakiwa wamekatwa viungo, ambapo asilimia 18 yao ni watoto.

Iliongeza kuwa familia 2,700 zimefutika kabisa na kuondolewa kwenye sajili ya kiraia, huku familia 6,020 zikiwa na mtu mmoja tu aliyebaki, na zaidi ya watoto 58,800 wamebaki yatima.

Israel imeharibu takriban asilimia 90 ya Gaza na sasa inakalia asilimia 80 ya ukanda huo, ikidondosha zaidi ya tani 223,000 za milipuko katika eneo hilo lenye msongamano mkubwa wa watu. Vita hivyo vimesababisha hasara ya moja kwa moja inayokadiriwa kufikia dola bilioni 80, ikiwemo dola bilioni 34 katika sekta ya nyumba pekee.

Ofisi ya vyombo vya habari iliripoti kuwa zaidi ya watu milioni 2.4 huko Gaza wamekumbwa na mauaji ya kimbari, njaa, na maangamizi ya kikaumu kwa siku 1,000. Zaidi ya familia 350,000 zinahitaji makazi, huku mahema zaidi ya 132,000 yakiharibiwa na zaidi ya Wapalestina milioni 2 wakiwa wamehama makazi yao.

Sekta ya afya imepata hasara kubwa, huku Israel ikiharibu au kusababisha hospitali 38 na vituo 96 vya afya kufungwa. Wagonjwa zaidi ya 22,000 wanahitaji matibabu nje ya nchi lakini wanazuiwa kusafiri, na zaidi ya watoto milioni 1.1 wanapata mlo mmoja tu kwa siku, jambo linalofafanuliwa kama sera ya kimfumo ya njaa.

Israel imeharibu misikiti 1,047 kabisa, imeharibu kwa sehemu mingine 210, imelenga makanisa matatu, na kuua viongozi 312 wa dini. Zaidi ya asilimia 87 ya ardhi ya kilimo imeharibiwa, na uzalishaji wa kila mwaka wa mboga na matunda umeshuka kutoka tani 524,000 hadi tani 20,000 pekee.

Harakati hizo za Palestina zimetoa wito wa mazungumzo mapana ya kitaifa ili kujenga upya taasisi za Palestina, ikiwemo Shirika la Ukombozi la Palestina (PLO), na kusisitiza hitaji la shinikizo kubwa zaidi la nchi za Kiarabu na Kiislamu ili kuulazimisha utawala wa Israel kuhitimisha kikamilifu mauaji ya kimbari.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa hali ya njaa imezidi kuwa mbaya kote Gaza, huku zaidi ya watu milioni 1.1 wakikabiliwa na uhaba wa chakula wa kiwango cha janga, kwani uingizaji wa misaada bado unazuiwa vikali na mzingiro unaoendelezwa na Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *