Arusha. Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (Esami), imezindua Kituo cha Umahiri cha Uchumi wa Afya na Utawala Afrika (AfriCHEG), kitakachosaidia nchi za Afrika kuimarisha mifumo ya afya kupitia sera zinazotegemea ushahidi, utafiti, mafunzo ya viongozi na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Kituo hicho kinatarajiwa kuongeza uwezo wa serikali na taasisi mbalimbali katika kuboresha ufadhili wa sekta ya afya, kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia ili kuharakisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Akizungumza leo Ijumaa, Julai 3, 2026 wakati wa uzinduzi huo jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa Esami, Profesa Peter Kiuluku amesema AfriCHEG imeanzishwa kuziba pengo kati ya tafiti na utekelezaji kwa kuhakikisha matokeo ya tafiti yanageuzwa kuwa sera na hatua zinazoweza kuleta matokeo yanayopimika.

“Dhamira yetu ni kuifanya AfriCHEG kuwa kituo bora cha umahiri barani Afrika katika uchumi wa afya, utawala, elimu ya viongozi, utafiti wa matumizi na ushauri wa kisera ili kusaidia nchi kujenga mifumo ya afya iliyo imara, yenye ustahimilivu na endelevu kifedha,” amesema.

Amesema kituo hicho kitatoa mafunzo kwa wataalamu wa afya katika maeneo ya matumizi ya Akili Unde (AI), uchambuzi wa takwimu, usimamizi wa fedha, manunuzi ya sekta ya afya pamoja na ufuatiliaji na tathmini ya programu mbalimbali.

Kwa mujibu wa Profesa Kiuluku, mafanikio ya sekta ya afya hayatategemea tu ujenzi wa hospitali au kuongeza watumishi, bali pia uongozi bora, matumizi sahihi ya rasilimali na maamuzi yanayotokana na ushahidi.

Amesema AfriCHEG pia itasaidia nchi za Afrika kuboresha upangaji wa huduma za afya, mifumo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, usimamizi wa fedha za umma pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali inayoongeza uwazi na ufanisi.

Aidha, kituo hicho kitakuwa jukwaa la ushirikiano kati ya serikali, vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kwa lengo la kuimarisha ubunifu na kuboresha sera za afya barani Afrika.

Mratibu wa AfriCHEG, Profesa Urbanus Kioko, amesema kituo hicho kimeanzishwa wakati ambapo Afrika inakabiliwa na changamoto mpya za afya, zikiwemo milipuko ya magonjwa kama Uviko 19 na Ebola pamoja na kuongezeka kwa usugu wa baadhi ya magonjwa.

“Serikali haziwezi kukabiliana na changamoto hizi peke yake. Ushirikiano kati ya wadau mbalimbali ni muhimu ili kujenga mifumo ya afya iliyo imara na endelevu,” amesema.

Naye Mtendaji Mkuu wa Velocity Project Management Ltd ya India, Hari Murthy amesema ushirikiano wa kimataifa utasaidia kubadilishana uzoefu, kufanya tafiti za pamoja na kutumia teknolojia nafuu za afya ili kuimarisha huduma kwa wananchi wa Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *