Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limezindua teknolojia ya nyumba janja (smart home) inayowawezesha wateja kufuatilia na kudhibiti vifaa vya umeme wanavyotumia nyumbani kwa kutumia simu za mkononi, hatua inayolenga kupunguza gharama za umeme, kuongeza usalama na kuhimiza matumizi bora ya nishati.

Ubunifu huo ni miongoni mwa teknolojia zinazooneshwa katika Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Shirika hilo linaonesha suluhisho za kidijitali zinazowapa watumiaji udhibiti zaidi wa matumizi ya umeme nyumbani.

Akizungumza katika maonyesho hayo leo, Ijumaa, Julai 3, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowello amesema suluhisho hilo la nyumba janja ni sehemu ya mkakati mpana wa shirika wa kuimarisha matumizi ya umeme kwa njia ya kisasa kadri Watanzania wengi wanavyopata huduma ya umeme wa uhakika.

Amesema teknolojia hiyo inalenga kuwasaidia pia wateja kutumia umeme kwa ufanisi zaidi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, huku ikiongeza urahisi na usalama wa nyumba.

“Wateja wanaweza kufuatilia matumizi ya umeme, kuwasha na kuzima vifaa kwa mbali, pamoja na kupanga vifaa kufanya kazi kwa muda maalumu. Hii inawapa udhibiti mkubwa wa matumizi yao na kusaidia kupunguza bili za umeme,” amesema.

Gowello ameongeza kuwa, mpango huo unaunga mkono ajenda ya Serikali ya nishati safi na mageuzi ya kidijitali kwa kuhimiza matumizi ya teknolojia zinazoongeza ufanisi wa nishati bila kupunguza ubora wa maisha.

Ofisa Masoko, Madeleine Shaidi, amesema mfumo huo unafanya kazi kwa kuunganisha vifaa vya nyumbani kama runinga, jokofu, viyoyozi, vipasha moto, vifaa vya kuchemshia maji na majiko ya umeme kwenye jukwaa la kidijitali kupitia programu ya simu iitwayo Smart Life.

Ameeleza kuwa wateja wanahitaji tu kufunga soketi na swichi janja zinazofanya kazi sambamba na mifumo ya kawaida ya umeme, hivyo kuepuka gharama kubwa za ujenzi upya.

“Baada ya vifaa kusimikwa, mwenye nyumba anaweza kudhibiti vifaa vyote vya umeme kutoka popote alipo kupitia simu iliyounganishwa na intaneti,” amesema.

Amesema programu ya Smart Life inawawezesha watumiaji kupanga vifaa kulingana na vyumba tofauti kama sebule, jiko na chumba cha kulala, hivyo kurahisisha udhibiti wa kila kifaa kwa mbali.

Zaidi ya udhibiti wa mbali, amesema teknolojia hiyo pia inawawezesha watumiaji kupanga ratiba za vifaa kuwashwa na kuzimwa kiotomatiki.

“Kwa mfano, taa za nje za ulinzi zinaweza kuwashwa wakati wa machweo na kuzimwa wakati wa macheo, huku hita za maji zikiwashwa kabla ya familia kuamka au kurudi nyumbani. Pia, mtu akisahau kuzima vifaa baada ya kutoka nyumbani, anaweza kufanya hivyo mara moja kupitia simu,” amesema.

Mfumo huo pia hutoa taarifa za kina za matumizi ya umeme, zinazomwezesha mtumiaji kufuatilia matumizi ya kila siku na ya kila mwezi na kubaini vifaa vinavyotumia umeme mwingi, hivyo kusaidia kufanya uamuzi sahihi ya kupunguza upotevu wa nishati.

Mtumiaji wa nyumba mahiri, Safari Fungo  amesema teknolojia hiyo ni hatua muhimu kuelekea maisha ya kisasa, akisema otomatiki inaweza kuongeza urahisi na ufanisi wa matumizi ya nishati.

Amesema sensa za mwendo zinaweza kuzima taa na viyoyozi kiotomatiki wakati vyumba havitumiki, huku mtumiaji akiwa na uwezo wa kuwasha vifaa kabla ya kufika nyumbani ili kuhakikisha starehe bila kupoteza umeme.

“Kwa nyumba mahiri, unaweza kupanga taa za nje kuwashwa wakati wa machweo na kuzimwa wakati wa macheo. Teknolojia hii inasaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya umeme huku ikirahisisha maisha ya kila siku,” amesema.

Fungo pia ametoa wito wa kuwepo kwa kanuni zitakazoruhusu nyumba zenye mifumo ya sola ya paa kurudisha umeme uliobaki kwenye gridi ya taifa kupitia mita za pande mbili, akisema mfumo huo utahamasisha uwekezaji zaidi katika nishati mbadala, sambamba na teknolojia za nyumba mahiri zinazolenga matumizi bora ya umeme.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *