Mufti na Mwenyekiti wa Baraza la Kidini la Waislamu wa Russia anaamini kuwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kiongozi shahidi wa Iran, wakati wa uhai wake alichukua hatua kubwa katika kuimarisha umoja na maelewano kati ya madhehebu ya Kiislamu.

Mufti Albir Khazrat Krganov amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na kueleza kwamba, baadhi ya watu katika nchi za Magharibi, hususan wataalamu wa masuala ya Uislamu, katika miongo ya hivi karibuni wamejitahidi kuibua mgawanyiko mkubwa kati ya Waislamu wa Sunni na Shia na kuonyesha tofauti hizo kana kwamba, ni ukuta usioweza kuvukwa, ilhali kwa hakika hali si hivyo.

Sheikh Krganov aliongeza kuwa harakati na juhudi za kiongozi shahidi wa Iran pamoja na wanazuoni wengine wakubwa, zilielekezwa katika kufichua juhudi za uongo zilizolenga kuwatenganisha Waislamu wa Shia na Sunni.

Mwanazuoni huyo wa Kisunni kutoka Russia akielezea kwamba hapo awali aliwahi kuhudhuria moja ya hotuba za kiongozi huyo shahidi mbele ya makundi mbalimbali ya wananchi wa Iran, alisema:

“Bila shaka, alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa wakiheshimiwa sana katika dunia ya leo; alikuwa mwanafikra aliyekuwa akizungumzia hali ya dunia kwa mtazamo wa dhamiri ya kibinadamu na kwa misingi ya elimu na maarifa ya dini.”

Mufti Krganov, akieleza kuwa maisha ya kidini ya familia na mtindo wa maisha wa unyenyekevu wa kiongozi shahidi wa Iran ni jambo linalofahamika vizuri, alisema:

“Aliondoka duniani kwa ujasiri na akapata daraja ya kufa shahidi. Hakujificha, hakukimbilia mafichoni wala kwenye mahandaki ya chini ya ardhi, bali alibaki katika ofisi yake ya kazi.”

Mufti Krganov aliongeza kuwa:

“Kiongozi shahidi wa Iran aliondoka duniani bila kushindwa. Alipata daraja ya kufa shahidi akiwa ni kiongozi mwenye nguvu na mwenye kuheshimiwa, ambaye Waislamu, hususan wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, walikuwa wakimwamini na kumtegemea.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *