
Muungano wa Kifungu cha 64, unaowaleta pamoja viongozi kadhaa wa upinzani, umeahirisha maandamano yake ya amani, ambayo awali yalipangwa kufanyika Julai 8, hadi Julai 22. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa, C64 ilitangaza kwamba imekubali mwaliko kutoka kwa Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, kwa ajili ya mashauriano kuhusu mgogoro wa kisiasa, usalama, na taasisi nchini DRC. Maelezo ya mpango huu bado hayajaeleweka.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu mjini Kinshasa, Pascal Mulegwa
Je, rais wa Burundi anashiriki kama mshirika wa Kinshasa au kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU)? Hata viongozi wa upinzani walioalikwa hawana majibu.
Jean-Marc Kabund alikuwa wa kwanza kuondoka Kinshasa siku ya Ijumaa jioni, siku mbili baada ya kupokea mwaliko huo. Viongozi wengine wa Muungano wa Kifungu cha 64 wanatarajiwa leo Jumamosi huko Gitega, mji mkuu wa kisiasa wa Burundi. Miongoni mwao ni Delly Sesanga, ambaye aliweza kupata pasipoti yake, ambayo ilikuwa imechukuliwa siku chache zilizopita na Kurugenzi Kuu ya Uhamiaji.
Mbali na C64, mwaliko huo pia ulitolewa kwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege, pamoja na Baraza Kuu la Maaskofu wa kanisa Katoliki nchini Kongo na Kanisa la Kristo nchini Kongo. Kambi ya Joseph Kabila, ambayo inapinga jukumu la Burundi katika mgogoro wa usalama mashariki, pia ilitangazwa kushiriki kikao hiki, lakini ilisema siku ya Ijumaa jioni kwamba haiijapewa mwaliko wowote.
Hawa wote ni wahusika wanaopinga marekebisho ya Katiba na wamekuwa wakitetea mazungumzo ya kitaifa jumuishi kwa miezi kadhaa.
Kulingana na taarifa zetu, mpango huu kutoka Gitega ulijadiliwa wakati wa ziara ya Évariste Ndayishimiye huko Kinshasa mnamo Juni 23.
Vyanzo vya serikali vinaelezea kwamba Burundi inatafuta kwanza kutathmini kiwango cha mgogoro wa kisiasa kabla ya kujihusisha zaidi. Wengine wanaona kama jaribio lingine la serikali ya Kongo, kufuatia ugumu uliopatikana katika kuileta Angola katika mashauriano yake ya kitaifa yaliyopendekezwa, ambayo yalijumuisha marekebisho ya katiba.