MAMIA ya washabiki wa Yanga wameendelea kujitokeza kwa wingi kwenye maeneo ya Karume, jijini, Dar es Salaam tayari kwa paredi la timu hiyo la kusherehekea ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu NBC.

Yanga inafanya paredi la ubingwa wa Ligi Kuu Bara leo Jumamosi Julai 4, 2026, baada ya kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani kutangazwa mabingwa wapya rasmi Juni 30, 2026, kufuatia kufikisha pointi 75 na kuwapiga bao watani zao wa jadi, Simba iliyomaliza nafasi ya pili na pointi zake 73.

Katika maeneo ya Karume jijini Dar es Salaam zilipo Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mashabiki wamejitokeza nje ya jengo hilo wakiwa na nyuso za furaha huku wakiimba na kucheza kwa pamoja.

Hata hivyo, Yanga ilitangaza shughuli hizo zingeanza tangu saa 4:00 asubuhi lakini hadi muda huu wa saa 5:18, bado hazijaanza rasmi wala gari maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya shamrashamra hizo halijafika pia.

Paredi hilo la Yanga ni mwendelezo wa mafanikio makubwa kwa kikosi hicho katika soka la Tanzania, baada ya kufikisha taji la 32, la Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *