DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala,Ridhiwani Kikwete amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kina nafasi ya kipekee katika kujenga na kuendeleza uwezo wa kiutendaji wa watumishi wa umma ambao ndio watekelezaji wa majukumu ya serikali kila siku.
Kikwete alisema hayo Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa chuo cha TPSC.
“Chuo hiki kina wajibu mkubwa wa kuhakikisha Watumishi wa Umma wanapata maarifa na stadi zinazolingana na mahitaji ya karne ya ishirini na moja ili kuwepo wa watumishi wenye sifa, ujuzi na uwezo wa kuongoza mabadiliko hayo,”alisema Kikwete.

Alisema serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika uimarishaji wa utumishi wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, za haraka na zenye tija.
Kikwete aliongeza kuwa,chuo hicho si tu taasisi ya mafunzo, bali ni nguzo muhimu ya serikali katika kujenga rasilimali watu yenye maarifa, stadi, maadili na uzalendo unaohitajika katika kutumikia umma kwa ufanisi.
Mkuu wa Chuo hicho,Dk Ernest Mabonesho alisema wanapoadhimisha miaka 25 ya chuo hicho wanajivunia mafanikio katika utoaji wa mafunzo, tafiti tumizi, ushauri wa kitaalamu na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kuimarisha utumishi wa umma.
Alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, TPSC kimeendelea kutekeleza dhamira ya serikali ya kujenga utumishi wa umma wenye ufanisi, weledi na unaozingatia matokeo.

Alieleza kuwa Chuo kimepanua huduma zake kutoka kampasi mbili hadi sita zilizopo Dar es Salaam, Tabora, Mtwara, Singida, Tanga na Mbeya, hatua iliyoongeza upatikanaji wa mafunzo nchini.
Alibainisja kuwa zaidi ya watumishi wapya 30,000 wamepata mafunzo elekezi ya awali, washiriki zaidi ya 104,797 wamenufaika na mafunzo ya uongozi, menejimenti na utawala, huku watahiniwa zaidi ya 22,555 wakifanya mitihani ya utumishi wa umma.
Alieleza katika mafunzo ya muda mrefu, Chuo kimeongeza programu kutoka kozi tatu za awali hadi astashahada, stashahada, shahada na shahada za uzamili.

Alisema udahili umeongezeka kutoka wanafunzi 185 mwaka 2002/2003 hadi zaidi ya wanafunzi 10,000 kila mwaka.
Aliongeza kuwa kwa upande wa tafiti, Chuo kimetekeleza shauri za kitaalamu 232, tafiti tumizi 55 na machapisho 122. Aidha, tafiti sita zilizofanywa katika kampasi zote sita zilizinduliwa rasmi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha tafiti zinazosaidia Serikali kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kisayansi.
Alieleza kuwa Chuo pia kimeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali, kupanua ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi pamoja na kuboresha miundombinu yake.
Akizungumzia mwelekeo wa miaka 25 ijayo, Mkuu wa Chuo alisema TPSC kitaendelea kuimarisha mafunzo kwa watumishi wa umma, matumizi ya teknolojia za kidijitali na Akili Unde, tafiti tumizi, ushirikiano wa kimkakati na miundombinu.
Alisema mafanikio ya miaka 25 ni msingi wa kuifanya TPSC kuendelea kuwa kitovu cha maendeleo ya rasilimali watu katika utumishi wa umma na mshirika muhimu wa Serikali katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.