NAIBU Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein, amesema gharama za kutumia viwanja vya michezo vinavyojengwa nchini ni miongoni mwa changamoto zinazowakwamisha vijana kunufaika na miundombinu hiyo.

Alisema, Serikali imewekeza katika ujenzi wa viwanja ili kukuza michezo na kuibua vipaji, lakini bado vijana wengi hushindwa kuvitumia kutokana na kutomudu ada za matumizi.

Kiongozi huyo alisema Serikali itaweka utaratibu utakaowezesha vijana kutumia viwanja hivyo kwa gharama nafuu ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unawanufaisha wananchi.

“Wizara inatambua kuna changamoto za vijana kutopata fursa za kutumia viwanja vinavyojengwa na serikali kwa kutomudu bei zilizopo, niwatoe hofu kuwa tunahitaji kutafuta ufumbuzi wa hilo,” alisema.

Alieleza kuwa, baadhi ya vijana wenye vipaji hukosa nafasi ya kufanya mazoezi mara kwa mara kwa sababu hawawezi kumudu ada zinazotozwa ili kutumia viwanja hivyo.

Alisema, anaamini endapo changamoto ya gharama itapatiwa ufumbuzi, viwanja vinavyojengwa vitatumika ipasavyo na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya michezo pamoja na kukuza vipaji vya vijana Zanzibar.

Naibu Waziri huyo alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya michezo kutafuta njia bora za kupunguza vikwazo vinavyowazuia vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za michezo.

Kwa mujibu wa wasimamizi wa uwanja wa Mao ulipo Unguja, matumizi yake kwa mchana gharama ya kukodi ni Sh100,000 huku usiku ikiwa Sh150,000, huku wadau wakilalamika gharama kubwa na kufanya baadhi kushindwa kumudu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *