Arusha. Edes Mlingi, aliyekuwa akipinga fidia ya Sh196.95 milioni aliyolipwa baada ya ardhi yake kuchukuliwa kwa ajili ya kupisha Mradi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), amekwama Mahakama ya Rufaa baada ya mahakama hiyo kuthibitisha kuwa alilipwa fidia kamili ya ardhi pamoja na maboresho yaliyokuwapo.

Mlingi alikata rufaa ya madai namba 797/2023 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamishna wa Ardhi, Msajili wa Hati, DART, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na Kampuni ya Puma Energy, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, uliotolewa Agosti 30, 2023.

Mahakama Kuu ilikuwa imetupilia mbali shauri lake kwa gharama, baada ya kubaini kuwa alilipwa kikamilifu fidia ya ardhi yenye ukubwa wa mita za mraba 1,632.

Mahakama hiyo ilisema baada ya kulipwa fidia hiyo, DART ilikuwa mmiliki halali wa mali iliyokuwa inabishaniwa.

Hukumu ya Mahakama ya Rufaa ilitolewa Julai 3, 2026 na jopo la Majaji Zephrine Galeba, Paul Kihwelo na Latifa Alhinai Mansoor na nakala yake ikiwekwa kwenye tovuti ya Mahakama.

Baada ya kupitia mwenendo wa shauri, hoja za rufaa na majibu ya pande zote, majaji hao walitupilia mbali rufaa ya Mlingi na kuthibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa katika shauri la ardhi namba 1/2020.

Mahakama pia ilimwamuru Mlingi kulipa gharama za rufaa kwa wajibu rufaa wa kwanza hadi wa tano, isipokuwa mjibu rufaa wa sita.

Msingi wa rufaa

Mlingi alikuwa mmiliki wa viwanja namba 491/1 na 493/1, Kitalu A, katika eneo la Manzese, Manispaa ya Ubungo, vyenye ukubwa wa mita za mraba 1,632, ambavyo alivinunua mwaka 2000.

Kutokana na upanuzi wa Barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni chini ya awamu ya kwanza ya mradi wa DART, Serikali ilichukua ardhi hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi. Baada ya tathmini kukamilika, Mlingi alilipwa fidia ya zaidi ya Sh196.95 milioni na DART.

Fidia hiyo ilihusisha thamani ya ardhi, jengo ambalo halikuwa limekamilika, uzio pamoja na posho mbalimbali. Hata hivyo, Mlingi hakuridhika akidai fidia hiyo ilihusu sehemu tu ya mali yake na si eneo lote, hivyo alikuwa mmiliki wa sehemu iliyobaki.

Kutokana na madai hayo, alifungua shauri Mahakama Kuu akiomba imtangaze kuwa mmiliki halali wa ardhi hiyo, izuie kuondolewa kwake kwenye eneo hilo na alipwe fidia zaidi. Mahakama Kuu ilitupilia mbali madai yake, hatua iliyomsukuma kukata rufaa Mahakama ya Rufaa

Mlingi aliwasilisha sababu tisa za rufaa, akidai Mahakama Kuu ilikosea kuhitimisha kuwa alilipwa fidia kamili kwa ardhi yote yenye ukubwa wa mita za mraba 1,632 wakati kwa madai yake, fidia ilihusu sehemu tu ya mali.

Alidai vielelezo vilivyowasilishwa, ikiwemo alama za ubomoaji kwenye jengo, Mfumo wa Sera ya Uhamishaji (RPF) na nyaraka nyingine, vilionyesha kuwa ni sehemu ya jengo pekee iliyokuwa imeathiriwa na mradi wa DART.

Pia alipinga Mahakama Kuu kutegemea ratiba ya fidia pekee bila kuzingatia ushahidi mwingine aliouwasilisha. Aidha, alidai mahakama ilikosea kuamini ushahidi wa mashahidi wa Serikali ambao, kwa maoni yake, ulikuwa na hitilafu na ulipingana.

Wajibu rufaa wa kwanza hadi wa tano waliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Camilius Ruhinda, ambaye alidai Mlingi alifungwa na maelezo yake mwenyewe ya madai yaliyokiri kuwa ardhi yake ilikuwa na ukubwa wa mita za mraba 1,632.

Alieleza kuwa hati ya fidia (Kielelezo D-1), ambayo ilisainiwa na Mlingi, ilithibitisha kuwa alipokea Sh196.95 milioni kama fidia ya ardhi yote (mita za mraba 1,632) pamoja na maboresho yaliyokuwapo.

Ruhinda alisema uthamini huo uliidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa sheria, huku uthamini binafsi wa Mlingi ukiwa haukuidhinishwa na hivyo kutokuwa na nguvu za kisheria.

Ameongeza kuwa ushahidi wa mashahidi wa Serikali haukuwa na mgongano, bali ulijengana na kuthibitisha kuwa mali yote ilinunuliwa kwa kuzingatia usalama wa jengo ambalo sehemu yake ingebaki baada ya utekelezaji wa mradi wa DART.

Kwa msingi huo, aliomba Mahakama ya Rufaa itupilie mbali rufaa hiyo na kuthibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu.

Katika uamuzi wake, Jaji Mansoor amesema baada ya kupitia rekodi ya shauri, vielelezo na hoja za pande zote, mahakama ilijiridhisha kuwa Mlingi alilipwa fidia kamili kwa ardhi pamoja na maboresho yote yaliyokuwapo.

Amesema Kielelezo D-1, kilichosainiwa na Mlingi, kinaonyesha kuwa malipo hayo yalihusu ardhi yote na maboresho yote yaliyokuwapo.

Mahakama imesema uthamini uliotumika uliidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa sheria, na Mlingi hakuwahi kuupinga kabla ya kupokea fedha hizo za fidia.

Imeongeza kuwa kitendo chake cha kuendelea kulipa kodi ya ardhi baada ya kulipwa fidia, hakiwezi kumpa haki ya kuendelea kudai umiliki wa eneo hilo.

Majaji walikubaliana pia na Mahakama Kuu kwamba ushahidi wa mashahidi wa Serikali haukuwa na mgongano kama alivyodai Mlingi, bali ulithibitisha kuwa uamuzi wa kuchukua mali yote ulifanywa kwa kuzingatia usalama wa jingo, ambalo sehemu yake ingebaki baada ya utekelezaji wa mradi.

“Mrufani hawezi kutangazwa kuwa mmiliki halali wa ardhi ambayo tayari alipokea fidia kamili. Kufanya hivyo kungekuwa sawa na kujinufaisha isivyo halali, jambo ambalo haliruhusiwi kisheria,” imesema sehemu ya hukumu.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama ya Rufaa ilihitimisha kuwa Mahakama Kuu ilitathmini ushahidi kwa usahihi na kutumia sheria ipasavyo, hivyo ikatupilia mbali rufaa hiyo na kumwamuru Mlingi kulipa gharama za rufaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *