
Vita vinavyoendelea nchini Sudan kati ya wanajeshi na wanamgambo wa RSF vimesabababisha kuwauwa kwa watoto 330 katika kipindi cha miezi sita ya mwaka huu.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Shirika la Umoja wa Mataifa, linaloshughulikia watoto UNICEF kupitia mwakilishi wake nchini Sudan Sheldon Yett, amesema watoto hao wanauawa na kujeruhiwa wakiwa nyumbani na barabarani.
Aidha, UNICEF inasema watoto hao wamekuwa wakiuawa wakiwa njiani kwenda shuleni au vituo vya afya, wakati huu pande zote zikiendelea kushambuliana.
Tangu kuanza kwa mwaka huu, watu zaidi ya Elfu moja wameuawa, asilimia 60 wakiwa ni watoto katika jimbo la Kordofan, huku mamilioni wakiendelea kukabiliwa na baa la njaa, wakiwemo 825,000 ambao wanasumbuliwa na utapiamlo.
Wakati hayo yakijiri, Mji wa El-Obeid, uliopo Kordofan Kaskazini, umeshuhudia ongezeko la mapigano, na kusababisha kuharibiwa kwa miundo mbinu muhimu kama za kuzalisha umeme, maji na shule.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, wapiganaji wa RSF wanajiandaa kutekeleza mashambulizi makubwa katika mji huo, hali inayotishia maisha ya watu zaidi ya Laki tano.
Tangu kuanza kwa vita Aprili mwaka 2023, maelfu ya watu wamepoteza maisha, huku mamilioni wakiyakimbia makaazi yao.