Nchome asisitiza kulinda amaniNchome asisitiza kulinda amani

DAR ES SALAAM: Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mwanga, Mchome Lemburus, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi.

Aidha amesisitiza zaidi watu kujiepusha na maandamano yasiyo na tija kwa taifa ambayo yanaweza kuchochea vurugu na kusababisha uharibifu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Julai 6, Lemburus amesema maandamano ni haki ya kikatiba inayopaswa kuheshimiwa, lakini yanapaswa kufanyika kwa amani bila kuharibu mali za umma.

Amesema vitendo vya uharibifu wa miundombinu kama vituo vya mabasi, vituo vya afya, shule na ofisi za umma hurudisha nyuma juhudi za maendeleo na kuwaathiri zaidi wananchi wa kawaida wanaotegemea huduma hizo.

Lemburus amewahimiza wananchi kutumia njia za amani, hekima na busara katika kutoa maoni na kudai haki zao, akieleza kuwa mazungumzo ndiyo njia bora ya kutatua changamoto kuliko vurugu na uharibifu wa mali.

Aidha, amesema mataifa mengi duniani yanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi, lakini suluhisho lake ni majadiliano na ushirikiano badala ya vitendo vya vurugu.

Pia amesisitiza kuwa CHADEMA inaamini katika misingi ya demokrasia na maendeleo, hivyo haipaswi kuhusishwa na vitendo vinavyoharibu miundombinu ya umma au kuvuruga amani ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *