SIMBA inafanya mambo yake kimyakimya na tayari imeshaanza kukusanya mastaa wa kigeni ikishusha kiungo mmoja wa kazi, akapewa mkataba kisha kutimka kuja kuanza kazi ya kuwatumikia wekundu hao kwa ajili ya msimu ujao.

Taarifa kutoka ndani ya Simba ambazo Mwanaspoti halina shaka nazo ni kwamba Simba imemshusha nchini kiungo Ibraheem Jabaar raia wa Nigeria, kisha kufanya mazungumzo yakumalizia  na mabosi wa klabu hiyo na baadaye staa huyo akapanda ndege na kuondoka zake.

Jabaar anatua Simba akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini ambayo ndio klabu aliyotokea kocha wa Wekundu hao Steve Barker wawili hao wakiwahi kufanya kazi pamoja kabla ya kuachana na sasa wanarudi kuungana tena.

Kiungo huyo mwenye miaka 23 ndiye aliyesajiliwa na Barker akiwa Stellenbosch lakini baada ya kuondoka kocha huyo na kuja Given Hunt ambaye alipunguza matumizi ya kiungo huyo kwenye klabu hiyo na kumfanya akose nafasi mara kwa mara.

NAFASI ZAKE

Jabaar kama atafanikiwa kuingia vizuri ndani ya Simba ataweza kuipa thamani kubwa klabu hiyo kutokana na uwezo wake wa kumudu kucheza nafasi nyingi ambapo mbali na kutumika kama kiungo mkabaji na mchezeshaji lakini anaweza kutumika kama beki wa kushoto na winga wa kushoto kama ikitokea dharura.

DAKIKA 802 BAO 1

Ndani ya Stellenbosch Jabaar amefanikiwa kucheza mechi 14 akitumia dakika 802, akifunga bao moja kwenye ushindi wa 1-0 nyumbani  na asisti kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Kaizer Chiefs, akitengeneza bao la pili likifungwa na mshambuliaji Titus Devon wakati timu yake ikishinda mabao 2-1 kwenye ligi kuu.

MKATABA WAKE SIMBA

Simba baada ya mazungumzo na Jabaar imempa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine ambapo alikuwa nchini kuanzia Simba ilipokuwa inacheza mechi ya mwisho dhidi ya KMC akiwa jukwaani wakati wekundu hao wakishinda kwa bao 1-0.

KAMARA NJE

Kiungo huyo mpya moja kwa moja anachukua nafasi ya Naby Camara ambaye Wekundu hao wamemsitishia mkataba mara baada ya ligi kumalizika,  kufuatia kukosa nafasi kwenye kikosi cha Barker akitumia muda mwingi jukwaani.

“Tumeshamalizana naye amesaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, Jabaar ni kiungo mzuri ambaye tutanufaika kwa kumtumia maeneo tofauti,”alisema bosi mmoja wa juu wa Simba.

Stellenbosch baada ya kuona Jabaar anakosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, ikakubali maombi ya kiungo huyo kusitisha mkataba wake akitaja kwamba hana furaha na maisha ya nchini humo kufuatia machafuko ya vita ya wazawa na wageni.

Jabaar ndiye anafungua dimba kwa usajili wa wachezaji wa kigeni baada ya Simba kutangulia kumalizana na wazawa watatu wakiwemo winga Ramadhan Chobwedo, kiungo Kelvin Nashoni na kiungo mshambuliaji Bakari Msimu.

DAKIKA 80 VS SIMBA

Msimu mmoja nyuma Jabaar alikuja nchini kucheza dhidi ya Simba kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo katika mechi ya kwanza wekundu hao wakiwa nyumbani walishinda kwa bao 1-0, alicheza kwa dakika 80 lakini mechi ya marudiano hakupata nafasi akikaa benchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *