BAADA ya kipa wa Simba, Yakoub Suleiman kufanyiwa upasuaji wa mguu wa kushoto takribani miezi miwili iliyopita, kwa sasa anaendelea vizuri akiwa chini ya uangalizi wa daktari.

Kaka wa kipa huyo, Mohamed Seif ‘Bello’ ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Polisi Dodoma katika msimu wa 2011-2012, alisema awali alikuwa anatembelea magongo mawili ila kwa sasa amebakia na moja na hali yake inaimarika siku hadi siku.

“Kwa sasa anatembelea gongo moja ambalo anaweza akaachana nalo pia siku za usoni, mara nyingi anaenda kupata maelezo ya daktari ya nini akifanye ili kuimarisha afya yake,” alisema.

Bello alisema baada ya Yakoub kufanyiwa upasuaji huo aliambiwa anaweza akakaa nje miezi sita hadi minane.

“Daktari alisisitiza miezi sita ni kama makadirio, lakini inaweza ikafika hadi nane, jambo la msingi ni Yakoub mwenyewe kuzingatia kile anachoambiwa na daktari anayemsimamia matibabu,” alisema.

Simba ilimsajili Yakoub baada ya kufanya vizuri akiwa JKT Tanzania ambapo msimu wa 2024-2025 alimaliza akiwa na ‘cleansheets’ nane.

Yakoub aliumia akiwa na timu ya Taifa Stars nchini Morocco, wakati ikijiandaa kucheza dhidi ya Nigeria mechi ya michuano ya AFCON 2025, Desemba mwaka jana.

Wakati huohuo beki Wilson Nangu kuendelea vizuri na kufanya mazoezi mepesi, baada ya kufanyiwa upasuaji Februari 2026 nchini Afrika Kusini.

Wachezaji wote wawili walisajiliwa na Simba wakitokea JKT Tanzania kwenye usajili mkubwa wa msimu uliopita lakini hakuweza kuwika kutokana na kukumbwa na majeraha hayo, wengine ambao wamekaa nje muda mrefu kwenye kikosi hicho ni Abdurazack Hamza na Moussa Camara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *