
Mamilioni ya waombolezaji leo walikusanyika katika mji mtakatifu wa Qom tangu asubuhi kushiriki katika mazishi ya Kiongozi Shahidi.
Barabara na maeneo ya wazi yalifurika watu waliowasili kutoka sehemu mbalimbali za Iran, katika tukio lililotajwa kuwa miongoni mwa misafara mikubwa zaidi ya mazishi kuwahi kufanyika katika mji huo.
Msafara wa kumuaga Kiongozi Shahidi ulianza katika Msikiti wa Jamkaran na kuelekea kwenye Haram ya Bibi Fatima al-Ma’suma (A.S), ukipitia barabara ya Rasul al-A’dham (s.a.w.) yenye urefu wa karibu kilomita saba. Njia hiyo ilifurika mamilioni ya waombolezaji waliofika kutoka maeneo mbalimbali ya Iran katika mji wa Qom, kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Kiongozi Shahidi na familia yake ya mashahidi.
Umati mkubwa wa waombolezaji uliendelea kuusindikiza mwili wa Kiongozi Shahidi kuelekea Haram ya Bibi Fatima al-Ma’suma (A.S), huku mazingira yakitawaliwa na huzuni na majonzi. Washiriki walikuwa wakitoa kaulimbiu za kidini na za mshikamano, wakionyesha uaminifu wao kwa viongozi wao. Picha za Kiongozi Shahidi na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei, zilibebwa na waombolezaji, huku bendera za maombolezo na bendera nyekundu zikipepea katika njia nzima ya msafara.
Wakazi wa mji mtakatifu wa Qom pamoja na wananchi waliowasili kutoka maeneo mbalimbali ya Iran na nchi nyingine walianza kujitokeza tangu usiku wa kuamkia leo, kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Imam Shahidi wa Umma. Tangu mapema jana alasiri, makundi ya wananchi kutoka Qom na mikoa mbalimbali yalielekea kwa miguu katika Msikiti wa Jamkaran, ambako yalishiriki katika hafla ya kuupokea mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi.”