Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alitarajiwa kusafiri kwenda Iraq leo Jumanne kuhudhuria shughuli ya mazishi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, iliyopangwa kufanyika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala kesho Jumatano.

Ziara hiyo inafanyika huku shughuli ya mazishi ya Kiongozi aliyeuawa shahidi na wanafamilia wake zikiendelea kote nchini Iran.

Msafara wa mazishi ya nchi nzima ulianza mapema Jumatatu hapa nchini, huku umati mkubwa wa mamilioni ya waombolezaji ukikusanyika kusindikiza majeneza ya Ayatullah Ali Khamenei, binti yake Sayyidah Bushra Husseini Khamenei, mkwewe Mesbahul Hoda Baqeri, mkamwana Zahra Haddad Adel (ambaye alikuwa mke wa Kiongozi wa sasa wa Mapinduzi ya Kislamu Mojtaba Khamenei), na mjukuu wake Zahra Mohammadi Golpayegani waliouawa katika shambulizi la kushtukiza katika siku ya kwanza na mashambulizi ya kigaidi ya Marekani na Israel mjini Tehran.

Jana jeneza la Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilisindikizwa na mamilioni ya waombolezaji katika shughuli ya kihistoria, na kubebwa kuelekea Uwanja wa Azadi mjini Tehran.

Wakiwa wamevaa nguo nyeusi na kujipiga vifua kwa huzuni, mamilioni ya Wairani na maelfu ya raia wa kigeni walioshiriki katika shughuli hiyo walijaa mitaani ya Tehran na kuruhusu wananchi kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa kihistoria wa taifa la Iran. Waombolezaji walitoa kaulimbiu zinazotaka kulipiza kisasi kwa damu ya Ayatullah Khamenei na kutangaza upinzani wao dhidi ya tawala za kibeberu huku wakipeperusha bendera za Iran.

Baada ya shughuli ya jana Jumatatu mjini Tehran, msafara wa mazishi leo uko katika mji mtakatifu wa Qum ambako mapema leo kumefanyika Swala ya Maiti iliyoongozwa na Ayatullah Abdullah Jawadi Amoli katika Msikiti wa Jamkaran. Keshi Jumatano, shughuli maalumu za kuaga na mazishi zitafanyika Najaf na Karbala, kabla ya mazishi ya mwisho kufanyika katika Haram ya mjukuu wa Mtume Muuhammad (SAW), Imam Ali bin Musa Ridha (AS) huko Mash’had, kaskazini mwa Iran, siku ya Alhamisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *