
Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeamuru uchunguzi wa haraka ufanyike kuhusu unyanyasaji unaoendelea katika mji wa al-Obeid nchini Sudan.
Baraza hilo limepitisha hoja ya kulaani machafuko yanayozidi kuongezeka yanayofanywa na wanamgambo wa kundi la RSF katika eneo la al-Obeid wakati wakianzisha uchunguzi wa dharura kuhusu madai ya unyanyasaji unaoendelea huko.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema afisa mkuu wa umoja huo anayeshughulikia masuala ya kibinadamu, Tom Fletcher, amezungumza kuhusu uhasama unaoongezeka katika mazungumzo ya simu na mkuu wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo.
Dujarric aliwaambia waandishi habari kwamba Dujarric alisema Fletcher alisisitiza umuhimu wa kudumisha ufikiaji salama kwa wahudumu wa kibinadamu na kuhakikisha harakati salama za raia, huku akielezea wasiwasi wake juu ya mashambulio ya ndege zisizo na rubani zinazoathiri raia na miundombinu wanayoitegemea.
Zaidi ya watoto 300 wameuawa au kujeruhiwa nchini Sudan katika kipindi cha miezi sita iliyopita, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) yakiwa chanzo kikuu cha vifo na majeraha hayo. Hayo yamefichuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia watoto (UNICEF) wakati mapigano yakizidi kuenea katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya Afrika.
UNICEF imesema kuwa mashambulizi ya droni na mizinga imelenga miundombinu ya kiraia, ikiwemo shule, masoko, vituo vya mafuta, na vituo vya maji, jambo ambalo limeweka zaidi ya watu 500,000 katika hatari kubwa ya maisha. Aidha, UNICEF imebainisha kuwa raia wamekuwa wakiteseka katika hali kutokana na mzingiro wa zaidi ya mwaka mmoja sasa.