Sambamba na kufanyika msafara wa mazishi ya Ali Khamenei, Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Tehran, macho ya ulimwengu mzima yalikuwa yameelekezwa Iran. Kilichofanyika mjini Tehran hayakuwa maombolezo tu bali lilikuwa tukio la kisiasa na kihistoria lililoakisiwa pakubwa kimataifa na vyombo vya habari.

Kuanzia alfajiri ya siku ya msafara wa maombolezo, makumi ya mitandao ya televisheni, mashirika ya habari na magazeti tajika ya kimaaifa yalirusha hewani moja kwa moja shughuli ya mazishi hayo yaliyowashirikisha mamilioni ya watu.

Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba hata vyombo vingi vya habari, ambavyo katika miezi ya hivi karibuni vimekuwa vikieneza habari za uongo kuhusu kutokuwepo utulivu na kudhoofika kwa Jamhuri ya Kiislamu baada ya vita, vimelazimika wakati huu kukubali ukweli tofauti, ukweli ambao umeonyesha hali halisi ya mambo uwanjani, ikishirikisha mamilioni ya waombolezaji, mipangilio mizuri ya mazishi na kuendelea kusimama imara mfumo wa uongozi nchini Iran, licha ya changamoto na mashinikizo kutoka kwa maadui. Suala hilihili ndilo limepelekea tukio hili licha ya kuwa la kidini na kitaifa, kuwa pia uwanja wa mashindano ya simulizi na kuarifishwa upya Iran katika vyombo vya habari vya kimataifa.

Tangu mwanzo wa siku ya maombolezo, vyombo vya habari vya kimataifa viliwatuma waandishi wao wa habari mjini Tehran na kupeperusha moja kwa moja tukio hili muhimu na hivyo kuibadilisha Tehran kuwa moja ya vituo muhimu vya habari duniani. Katika uchanganuzi nadra na usio wa kawaida, Reuters iliandika kwamba msafara wa mazishi ulikuwa zaidi ya tukio la kitaifa la kuaga mwili wa kiongozi wa taifa, ambapo bahari ya mamilioni ya waombolezaji mjini Tehran ilituma ujumbe wa wazi kwa Marekani na utawala wa Kizayuni kwamba juhudi zao za kujaribu kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilikuwa zimegonga mwamba na kushindwa. Shirika hilo la habari lilisisitiza kwamba, baada ya vita, Iran si tu haijadhoofika bali imeonyesha ustahimilivu mkubwa na umoja wa kitaifa, ikidhihiri kuwa mshindi mkubwa mkubwa aliye tayari kuwa na nafasi muhimu zaidi katika mfumo mpya wa eneo.

BBC ya Kiarabu pia imeangazia pakubwa mazishi hayo na kutaja tukio hilo kama “la kihistoria” na kuripoti kwamba msafara huo ulienea kwa umbali wa makilomita kadhaa katika mitaa ya Tehran.

Shirika la AFP pia lilichambua mahudhurio hayo makubwa ya umma kama ishara ya ustahimilivu wa Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni, likisema kuwa idadi ya washiriki inaweza kulingana au hata kuzidi ile ya msafara wa mazishi ya mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Mashirika ya The Associated Press, ABC News, Euronews, na TRT ya Uturuki pia yaliripoti kwa kina kuhusu umati mkubwa wa watu, hali ya hisia kali katika mazishi, na ushiriki mkubwa wa matabaka mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni yaliyoshiriki kwenye mazishi.

Katika nyanja ya vyombo vya habari vya kikanda, vituo kama vile Al Jazeera, Al-Manar, Al-Masirah, Al-Ahad, na Shahab ya Palestina pamoja na mitandao ya Iraq na Lebanon, vilirusha matangazo ya moja kwa moja ya mazishi hayo, huku vikielezea kujitokeza kwa mamilioni ya watu kama kipengee muhimu zaidi cha tukio hilo.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Russia, ikiwa ni pamoja na RIA Novosti na TASS, viliripoti kwamba, kuanzia mapambazuko, mitaa ya Tehran ilikuwa imefurika umati wa watu waliokuwa wamekusanyika kumuaga kiongozi wao aliyeuawa shahidi.

Hata vyombo vya habari vinavyohusishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, kama The Times of Israel, Jerusalem Post na Haaretz, havikuweza kufumbia macho wingi wa watu waliojitokeza kumuaga kiongozi wao katika mitaa ya Tehran.

Nukta ya pamoja iliyoashiriwa na vyombo hivyo vyote ni kuhusu umoja na mshikamano wa ndani na kuendelea kuimarika mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Katika miezi ya hivi karibuni, baadhi ya chambuzi za Magharibi zilidai kwamba kuondolewa kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi kungeweza kufungua njia ya kutokuwa na utulivu wa kisiasa na mpasuko ndani ya muundo wa madaraka nchini, lakini picha zilizoonyeshwa kutoka Tehran zimewasilisha simulizi tofauti kabisa mbele ya maoni ya umma kimataifa.

Ukweli huu haukuakisiwa tu na vyombo vya habari. Glenn Greenwald, mwandishi wa habari wa Marekani na mshindi wa Tuzo ya Pulitzer, amesambaza picha za mazishi hayo na kusema ni vigumu kutasawari umati mkubwa kama huo ukikusanyika kwa ajili ya mazishi ya kiongozi nchini Marekani.

Max Blumenthal, mwandishi wa habari wa Marekani, pia ameelezea mazishi hayo kama moja ya nyakati za kudumu milele katika harakati za kupinga ubeberu, akisisitiza kwamba ikiwa lengo la mauaji ya Kiongozi wa Mapinduzi lilikuwa kubadili mfumo wa kisiasa wa Iran, picha kutoka Tehran leo zimeonyesha kwamba mkakati huu umefifia na kufeli.

Matamshi haya, sambamba na ripoti za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, yanaashiria kuwa vita vya kifikra vinavyoendeshwa dhidi ya Iran hukabiliwa na changamoto pindi vinapokabiliana na hali halisi nyanjani.

Wakati huo huo, uwepo mjini Tehran wa jumbe nyingi za kigeni, matangazo ya moja kwa moja na makumi ya vyombo vya habari vya kimataifa, na pia kufanyika mazishi hayo nchini Iraq umetilia nguvu ukweli kwamba tukio hili limevuka mipaka ya Iran, na kuwa la kikanda, na hata la kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *