
WAKATI Leonard Thadeo akivunja ukimya baada ya kutangazwa kuwa rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Anthony Mtaka amesema anasubiri ripoti ya Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC).
IOC ilimtuma mwakilishi, Dk Donald Rukare kufuatilia uchaguzi huo uliofanyika Julai 5, 2026 jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, hali ya sintofahamu iliibuka kufuatia wapiga kura kugomea matokeo yaliyotangazwa na Kamisheni ya Uchaguzi huo kumpa ushindi Thadeo wakidai hawajamchagua huku wakilalamikia matokeo kuwa kinyume nyume.
Kamisheni ya uchaguzi ilimtangaza Thadeo, mkurugenzi mstaafu wa maendeleo ya Michezo na Katibu Mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuwa ndiye mshindi kwa kura 19 kati ya 36 zilizopigwa.
Kamisheni hiyo ilisema Mtaka amepata kura 11 na Henry Tandau makamu wa rais mstaafu wa TOC amepata kura sita kwenye nafasi ya urais, matokeo yaliyopingwa vikali na wajumbe wakidai Thadeo aliyetangazwa mshindi alipata kura moja na Mtaka kura 29, lakini imetangazwa kinyume nyume.
Baada ya sintofahamu hiyo, washindi waliotangazwa na Kamisheni ya uchaguzi hawakuapishwa hadi jana Julai 6, 2026 walipoapishwa chini ya usimamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Akizungumzia sintofahamu hiyo, Mtaka ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Njombe amesema taratibu hazikupaswa kuwa hivyo zilivyokuwa.
“Pale ukumbini kulikuwa na mtu IOC ameona kilichotokea, atapeleka taarifa ya alichokishuhudia, jambo ambalo litatuletea picha mbaya,” amesema.
Amesema mwakilishi wa IOC ameona kilichotokea na “waliopindua” matokea wangeweza kufanya hivyo kama kura zimehesabiwa chumbani, lakini kura zilihesabiwa hadharani.
“Wote waliokuwa pale wanafahamu aliyetangazwa mshindi kapata kura moja, Mtaka kapata 29 na Tandau kura 6, wacha tusubiri ripoti ya IOC kwanza,” amesema Mtaka.
Akizungumzia ushindi wake, Thadeo amesema baada ya kuapishwa jana Jumatatu, leo ni siku kuu ya Sabasaba hivyo wanasubiri taarifa kwa uongozi uliomaliza muda lini watakuwa tayari kwa makabidhiano ya ofisi.
“Wakati wa uchaguzi nilikuwa na vipaumbele vyangu, nimepata uongozi sio vyangu tena ni vya TOC, hivyo baada ya uchaguzi tutakwenda kuviunganisha na kuwa vipaumbele vya timu kwa ajili ya kuipeleka mbele Kamati ya Olimpiki,” amesema.
Kuhusu sintofahamu iliyotokea kwenye uchaguzi na wajumbe wengi kumkataa kwamba hawajamchagua, Thadeo amesema hayo yanaweza kuzungumzwa na Kamati ya uchaguzi na sio yeye.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchaguzi huo, Ibrahim Mkwawa alipoulizwa alijibu kwa kifupi anayetakiwa kuulizwa sintofahamu hiyo ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
“Mimi nilishamaliza kazi yangu, maswali aulizwe BMT waliowaapisha,” amesema Mkwawa kwa kifupi leo Julai 7, 2026 alipozungumza na Mwananchi.
Mwananchi ilimtafuta mwakilishi wa BMT aliyekuwepo kwenye uchaguzi huo, Maguzu ambaye amesema anayeweza kuzungumzia hilo ni bosi wake, Neema Msitha ambaye ni Katibu Mkuu.
Neema ambaye yupo nchini Ufaransa alipotafutwa kwa WhatsApp, simu yake haikupatikana.