Kamisheni ya Kiswahili ya Muungano wa Afrika, (AU) kwa kifupi ACALAN-Kiswahili itajenga makao yake makuu nchini Uganda katika jitihada za kuhakikisha kuwa lugha hiyo inaimarika barani Afrika.

Hayo yamedokezwa na Profesa Pacifique Malonga kutoka Rwanda, ambaye ni Kamishna katika Kamisheni ya Kiswahili ya Muungano wa Afrika.

Profesa Malonga amesema kuwa, “yeyote atakayesema kwamba Kiswahili kilifia Uganda, basi aongeze kwamba pia kilifufuliwa tena Uganda.” 

Kwa mujibu wa Prof. Malonga, mipango ya kujenga makao makuu ya ACALAN Kiswahili nchini Uganda ni ishara kuwa lugha ya Kiswahili itaendelea kukua na kuenea zaidi barani Afrika na duniani.

Amesema:”Nakumbuka miaka 15 iliyopita tulipopitisha ACALAN Kiswahili, nilikuwa bado kijana mjini Nairobi. Leo ni siku ya furaha kuona Kiswahili kikiendelea kuenea.”

Katibu Mkuu wa ACALAN Kiswahili, Dkt. Ronex Kisembo Tendo, amesema Makao Makuu ya kamisheni hiyo yanatarajiwa kujengwa jijini Kampala ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa kamisheni mpya.

Dkt. Kisembo amesema: “Natumaini kwamba Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, atawashawishi marais wenzake kuunga mkono ujenzi wa makao makuu ya ACALAN Kiswahili hapa Uganda.”

Kwa upande wake, Prof. Aldin Mutembei wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye ni Mratibu wa ACALAN Kiswahili, amesema huu ni wakati wa vijana kujifunza Kiswahili kwa mkakati ili wanufaike na fursa zinazozidi kuongezeka barani Afrika na duniani.

Kila mwaka tarehe 7 Julai huadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili, iliyoanzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2021 kwa kutambua mchango wa lugha hiyo katika kuimarisha mshikamano, mawasiliano na kuhifadhi pamoja na kubadilishana tamaduni duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *