Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) anasema kuwa sekta ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu imefikia kiwango chake cha sasa cha maendeleo kupitia mwongozo na uungaji mkono thabiti wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Katika mahojiano ya televisheni siku ya Jumanne, Mohammad Eslami amesema kuwa sera za kistratijia za muda mrefu zilizoundwa chini ya uongozi wa Kiongozi Shahidi ndizo ziliweka msingi wa maendeleo ya teknolojia ya nyuklia na uzalishaji wa nishati nchini.

Amebainisha jinsi Iran ilivyozidi kupiga hatua kwa kufuata sera hizo, licha ya juhudi endelevu za maadui za kutaka kuzuia maendeleo ya nchi.

Amesisitiza: “Licha ya vizuizi na matatizo yote ambayo maadui wa Iran wameyaibua ili kuzuia nchi kufanikiwa, na licha ya operesheni nyingi walizozifanya tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa neema ya Mwenyezi Mungu, lengo hili, yaani maendeleo ya nchi, limetimizwa, na hadhi ya Iran imebadilika.”

Akirejelea maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya nchi, Eslami amesema kuwa Kiongozi Shahidi alikuwa amesimama kidete kuziunga mkono sekta za kistratijia, ikiwemo teknolojia ya nyuklia, tangu mwanzo.

Eslami amesema Kiongozi Shahidi alisisitiza kwanza haja ya kufikia uwezo wa megawati 20,000 za umeme wa nyuklia mnamo 2007, akilielezea lengo hilo kama kipaumbele endelevu cha kitaifa.

Amesema kuwa kitengo cha kwanza cha Kituo cha Nishati ya Nyuklia cha Bushehr kusini mwa Iran kinafanya kazi kwa sasa, huku ujenzi wa vitengo vya pili na vya tatu vya kituo hicho ukiendelea.

Kulingana na Eslami, mipango imeandaliwa pia ya kujenga vituo zaidi vya nishati ya nyuklia kando ya ukanda wa pwani ya kusini mwa Iran, katika Mkoa wa Khuzestan, ambao pia uko kusini, na Mkoa wa kaskazini wa Golestan, huku tafiti za kimazingira zikiwa zimekamilika kwa kiasi na miradi sasa ikiingia katika awamu ya mikataba.

Eslami amehitimisha kwa kusema kuwa mpango wa nyuklia wa Iran unavuka mipaka ya uzalishaji wa umeme kwani umejikita pia katika huduma za afya kupitia uzalishaji aina ya radiopharmaceuticals.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *