Kampeni hiyo imeandaliwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS kwa ushirikiano na serikali ya jimbo. Lengo ni kuimarisha maridhiano, mshikamano wa kijamii na kuhimiza vijana kuwa mstari wa mbele katika kujenga amani. Feissal Kirwa kupitia video ya UNMISS amefuatilia uzinduzi huo na sasa anatuletea mada hii kwa kina. 

Ngoma za asili zimetamalaki hapa Yambio, mji mkuu wa jimbo la Equitoria Magharibi nchini Sudan Kusini. Kikundi cha watoto kiko makini kabisa kinatumbuiza..

Kisha watu wazima nao, wanawake kwa wanaume pamoja na vijana wako kilingeni, mpiga ngoma naye yuko makini midundo iende sambamba na walio kilingeni.

Ni shangwe na nderemo kwenye uzinduzi wa kampeni ya Tusikilizeni, Chukueni Hatua sasa hapa Yambio, zikiwa na ujumbe wa matumaini na umoja badala ya kumbukumbu za migogoro inayoendelea kughubika eneo hili la Sudan Kusini.

UNMISS Mwanafunzi wa kike anakariri shairi la amani katika hafla rasmi ya kukuza amani nchini Sudan Kusini.

Vijana, wazee, viongozi wa dini na wa kimila, wanawake, wasanii pamoja na viongozi wa serikali wanakusanyika kusherehekea uzinduzi wa kampeni inayolenga kujenga utamaduni wa mazungumzo, maridhiano na amani ya kudumu.

Kupitia muziki, ngoma na maonesho ya kitamaduni, jamii zinaonesha utofauti wao huku zikithibitisha dhamira ya pamoja ya kuishi kwa amani. 

Video sasa inamleta katikati mtoto Gamboripai Flora, akiwa amepiga magoti na kipaza sauti mkononi, kwa mtindo wa ngonjera akatoa ujumbe kwa niaba ya watoto wengi waliokumbwa na madhara kutokana na mgogoro unaoendelea.

“Amani! Tumekuwa tunakutafuta usiku na mchana Umekuwa wapi siku zote? Njoo ukae nasi. Njoo utuongoze.”

Kisha tukaelekezwa jukwani, vijana wakitumbuiza, wananchi wakishangilia na kupunga mikono kuunga mkono ujumbe wa amani.

Kwa wanawake wengi, amani si tu matarajio, bali ni jukumu. Baada ya kubeba mzigo mkubwa wa madhara ya mzozo, wanawake hao wanazitaka familia na jamii kukataa vurugu na kukumbatia mazungumzo kama njia ya maridhiano. Flora Gume, mwanachama wa Umoja wa Wanawake jimboni Equitoria Magharibi anafunguka.

“Tunapaswa kutambua kwamba amani inaanzia kwa wanawake. Hawa ni akina mama na ndio walioathirika zaidi vibaya na migogoro. Ikiwa sisi ni wajenzi wa kweli wa amani, tunapaswa kuzungumza na waume wetu, watoto wetu na vijana wetu, tuwahimize kuweka silaha chini na kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo.”

Video inatuonesha washiriki wakifuatilia hafla, na viongozi wa jamii wakizungumza na wananchi.

Kwa mujibu wa viongozi wa asasi za kiraia, vijana wamekuwa upande wa migogoro, lakini sasa wanaonesha utayari wa kuwa sehemu ya suluhisho. Emmanuel Wanga, mwanachama wa MTandao wa Asasi za Kiraia anafafanua.

“Kwa muda mrefu vijana walitumika kuchochea migogoro. Wamepoteza muda mwingi na kupotoshwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa. Lakini sasa wanapoongoza kutoa wito wa amani, hiyo ni ishara ya mabadiliko. Kilichobaki ni kuimarisha ushirikiano kati ya raia na vyombo vya usalama kwa msaada wa serikali.”

Maonesho ya kitamaduni yakiendelea huku wananchi wakishiriki kwa shangwe, Emmanuel Dukundane, Afisa wa Masuala ya Kiraia, UNMISS anasema kampeni ya ” Tusikilizeni, Chukueni Hatua sasa “ inalenga kuhakikisha kila sauti inasikika, hususan sauti za vijana, ili ziwe sehemu ya juhudi za kujenga amani ya kudumu.

“Kampeni ya Tusikilizeni, Chukueni Hatua sasa  inaonesha dhamira ya pamoja ya kuhakikisha kila sauti, hususan za vijana, zinasikika na zinachangia juhudi za kujenga amani yenye matokeo ya kudumu.”

Sauti za ngoma zikififia huku washiriki wakimalizia maonesho ya kitamaduni, ujumbe wa amani unaendelea kuishi. Kwa ushirikiano na Wizara ya Utamaduni, Vijana na Michezo ya Jimbo la Equatoria magharibi, UNMISS inapanga kupeleka kampeni ya Tusikilizeni, Chukueni Hatua sasa “ katika kaunti mbalimbali za jimbo hilo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Lengo ni kuendelea kuhamasisha mazungumzo, maridhiano na mshikamano wa kijamii, huku vijana wakipewa nafasi ya kuwa nguzo muhimu katika kujenga Sudan Kusini yenye amani na maendeleo ya kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *