Dar es Salaam. Watanzania wiki hii wanaanza kununua saruji kwa bei ya juu zaidi baada ya wazalishaji wakubwa kutangaza marekebisho ya bei, hatua inayotarajiwa kuongeza gharama katika sekta ya ujenzi.

Marekebisho hayo yanatarajiwa kuongeza bei ya mfuko mmoja wa saruji kufikia kati ya Sh17, 000 na Sh18,150, kutegemea aina ya saruji, eneo la mauzo na gharama za wasambazaji wake.

Ongezeko hilo linatokana na wazalishaji kutangaza kupandisha bei kwa kati ya Sh500 na Sh650 kwa mfuko mmoja, kabla ya kuongezwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Hatua hiyo imekuja baada ya kampuni kadhaa za saruji kutoa matangazo kati ya Julai 3 na 6, 2026, zikieleza kuwa mabadiliko hayo yamesababishwa na kupanda kwa gharama za uzalishaji, malighafi, usafirishaji, kodi na gharama nyingine za uendeshaji.

Ongezeko hilo latarajiwa kuongeza gharama za ujenzi kwa wananchi, makandarasi na waendelezaji wa majengo na miradi mikubwa ya miundombinu

Kampuni ya Saruji ya Dangote imetangaza kuongeza bei kwa Sh650 kwa mfuko wa kilo 50 bila VAT kwa aina zote za saruji zinazozalishwa na kampuni hiyo, ikiwamo 32.5R, 32.5N, 42.5N, 42.5R na 52.5N.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, marekebisho hayo yametokana na ongezeko la majukumu ya kifedha, gharama za kisheria, ununuzi wa malighafi na gharama za jumla za uendeshaji.

Nayo Moshi Cement, inayomilikiwa na Jun Yu Investment International Company Limited, imetangaza kuongeza bei kwa Sh500 kwa mfuko mmoja, ikitaja kupanda kwa gharama za malighafi na usafirishaji.

Baadhi ya wazalishaji wametangaza mabadiliko ya bei kwa kuzingatia tani badala ya mifuko.

Maweni Limestone Limited (Huaxin) imeongeza bei kwa Sh13,000 kwa tani bila VAT kwa saruji inayozalishwa katika viwanda vyake vya Tanga na Mkuranga, ikieleza kuwa hatua hiyo imesababishwa na ongezeko la gharama za uzalishaji na matengenezo ya mitambo.

Tanga Cement PLC (Simba Cement) nayo imetangaza ongezeko la Sh13, 000 kwa tani, ikitaja kupanda kwa gharama za kodi, pembejeo na uendeshaji wa biashara.

Lake Cement Limited, wazalishaji wa Saruji ya Nyati, pia imetangaza ongezeko la Sh13, 000 kwa tani kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na usafirishaji.

Mbeya Cement Company Limited imefanya marekebisho kulingana na aina ya bidhaa, ambapo Fastaplus 32.5 imeongezeka kwa Sh9, 085 kwa tani, huku Tembo Supaset 42.5 na Tembo Powerplus 42.5N ikiongezeka kwa Sh14,136 kwa tani.

Kodi zatawala mjadala

Mabadiliko hayo ya bei yamekuja wakati Serikali ikianza kutekeleza marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa katika mwaka wa fedha 2026/27.

Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, wakati akiwasilisha Bajeti ya Taifa, alisema Serikali itaongeza viwango vya ushuru maalumu wa bidhaa kwa asilimia nane mwaka huu wa fedha, badala ya utaratibu wa awali wa kufanya ongezeko kubwa kila baada ya miaka mitatu.

Alisema hatua hiyo inalenga kuakisi thamani halisi ya mapato ya Serikali, kuweka mfumo wa kodi unaotabirika na kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Marekebisho hayo yanatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa takribani Sh251.54 bilioni.

Wazalishaji wa saruji wamekuwa wakitaja kodi na tozo mbalimbali za kisheria kuwa miongoni mwa sababu zinazoongeza gharama za uzalishaji.

Uzalishaji wazidi mahitaji

Ongezeko la bei limekuja wakati Tanzania inatajwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa saruji, unaozidi mahitaji ya ndani.

Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, Tanzania ina viwanda 15 vya saruji vyenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 13.6 kwa mwaka.

Alisema hadi Aprili 2026, viwanda hivyo vilikuwa vimezalisha takribani tani milioni 10.3 za saruji, wakati mahitaji ya ndani yakikadiriwa kuwa tani milioni 8.5 kwa mwaka.

Ziada ya saruji husafirishwa katika masoko ya nchi jirani kama Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi.

Sekta ya saruji inatajwa kutoa ajira takribani 6,020 za moja kwa moja na ajira 20,280 zisizo za moja kwa moja.

Aidha, kiwanda kipya cha WIH Holding Limited kilichopo Mkoa wa Kigoma kimeongeza uwezo wa uzalishaji nchini.

 Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.9 kwa mwaka na hadi Aprili 2026 kilikuwa kimezalisha takribani tani milioni 1.5.

Mabadiliko haya yanaweka mtihani mpya katika jitihada za Tanzania za kukuza sekta ya viwanda, ikiwa ni kuona kama ongezeko la uzalishaji litaweza kusaidia kupunguza gharama kwa walaji au kama shinikizo la kodi na gharama za uendeshaji litaendelea kuongeza bei ya bidhaa hiyo muhimu katika ujenzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *