Dar es Salaam. Ili kurahisisha kufikia uchumi wa kidijitali, matumizi ya simu janja yameendelea kuwa moja ya nyenzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika huduma za kifedha, biashara mtandaoni, elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa.
Hata hivyo, pamoja na ongezeko la matumizi ya teknolojia nchini, bado kuna pengo kubwa la upatikanaji wa simu janja huku baadhi ya Watanzania wakiendelea kutumia simu za kawaida ambazo zinawanyima fursa ya kutumia kikamilifu huduma zinazotolewa kwenye mifumo ya kidijitali.
Ili kutimiza azma ya kujenga Tanzania ya kidijitali, kampuni ya mawasiliano ya Halotel kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia ya Samsung imeanzisha mpango wa kuwawezesha Watanzania kupata simu janja kwa mfumo wa mkopo, hatua inayolenga kuongeza idadi ya wananchi wanaoweza kumiliki vifaa hivyo kwa urahisi.
Mpango huu unakuja wakati ambao takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania hutumia mifumo hii ya simu kufanya miamala yao ya kila siku kwa urahisi
Kupitia ushirikiano huo, Samsung imeleta aina mbalimbali za simu zake za kisasa zikiwemo Galaxy A07, A06 na A17 ambazo zitapatikana katika mtandao wa maduka ya Halotel nchini kote, huku wateja wakipewa fursa ya kulipa kwa awamu kulingana na uwezo wao.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Meneja wa Biashara wa Samsung Electronics Tanzania, Daesong Ra, amesema ushirikiano huo unaendana na mkakati wa kampuni hiyo wa kupanua upatikanaji wa teknolojia nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Amebainisha kuwa Samsung imejipanga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata simu halisi za kampuni hiyo kupitia mfumo wa mikopo unaowezesha malipo ya taratibu, huku wakifurahia huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu.
Amesema Samsung inalenga kuhakikisha upatikanaji wa simu hizo hauishii mijini pekee, bali unawafikia wananchi waliopo maeneo mbalimbali nchini kupitia mtandao wa usambazaji wa Halotel na Samsung.
“Tunataka kuhakikisha kwamba Mtanzania yuko Kigoma, yuko Musoma au yuko sehemu yoyote nchini ana uwezo wa kupata simu ya Samsung wakati wote kwa bei nafuu,” amesema.
Kwa mujibu wa Samsung, simu zitakazotolewa kupitia mpango huo zitakuwa na dhamana ya miaka miwili ambapo wateja wataweza kupata huduma za matengenezo bila malipo endapo simu zao zitapata hitilafu ndani ya kipindi hicho.
“Ukikinunua simu leo, kwa miaka miwili simu yako ina warranty. Chochote kitakachotokea kwenye simu hiyo unaenda kwenye service centre (vituo vya matengenezo) ambazo zipo zaidi ya 70 nchi nzima na utafanyiwa matengenezo bure,” amesema.
Amesema tofauti nyingine ya mpango huo ni kuunganishwa kwa huduma za mkopo kutoka Halotel, jambo litakalowawezesha wananchi kumiliki simu janja bila kulipa gharama yote kwa wakati mmoja.
“Hiki ni kitu ambacho ni bora kabisa. Tunahakikisha tunamfikia Mtanzania popote alipo,” amesema.
Mkurugenzi wa Biashara wa Halotel, Abdallah Salum, amesema ushirikiano huo mpya utachochea maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini kwa kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumiliki simu janja.
Amesema mpango huo pia utaimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kupitia teknolojia za kisasa na huduma bunifu zinazotolewa na kampuni hiyo.
Huduma hiyo mpya itawawezesha wateja wanaokidhi vigezo kumiliki simu janja za Samsung kwa malipo ya awamu, jambo linalotarajiwa kuongeza matumizi ya simu janja miongoni mwa wanafunzi, vijana, wajasiriamali na familia mbalimbali nchini.