Dar es Salaam. Hadi lini? Ndilo swali linalogonga vichwa vya wadau wa kada mbalimbali kuhusu mwenendo wa matishio ya kiusalama yanayoibuka mara kwa mara, kusimamisha shughuli za kiuchumi, kisiasa na kuibua hofu kwa wananchi.

Swali hilo linaibuka kwa sababu si mara ya kwanza hali kama hiyo kutokea. Kuliibuka tishio la maandamano Desemba 9, mwaka jana, likasimamisha shughuli za kiuchumi, askari wakasambazwa mitaani na hofu ikawajaa wananchi, hata hivyo hayakufanyika.

Hilo limejirudia Julai 7, mwaka huu, ambapo wanaharakati kupitia mitandao ya kijamii waliitisha maandamano nchi nzima. Shughuli za kiuchumi zilisimama katika majiji kadhaa na askari wakamwagwa mitaani.

Jioni ya Leo Julai 7, 2026 wananchi mkoani Songwe katika maeneo tofauti tofauti wakiendelea na shughuli zao kama kawaida. Picha na Denis Sinkonde

Hofu zote hizo, ikiwemo kusambazwa kwa askari, zinasababishwa na kilichotokea Oktoba 29, mwaka jana. Kuliibuka matishio ya maandamano, yakafanyika na kuibua vurugu zilizosababisha mauaji, uharibifu wa mali za umma na watu binafsi.

Kwa sababu matishio yamekuwa yakijirudia na wasiwasi unaibuka, wadau wa kada mbalimbali wanasema ni wakati wa Serikali kutatua tatizo kwa kuanzia kwenye mzizi, ili kuwe na uendelevu wa utulivu nchini.

Wengine wanasema kuendelea kwa matishio, hofu na wasiwasi kunapoteza imani ya wawekezaji kuwekeza mitaji yao katika Taifa ambalo amani yake haitabiriki.

Dhamira ya matishio hayo yanadaiwa kushinikiza kupatikana kwa Katiba Mpya, mabadiliko ya sheria za uchaguzi, kurudiwa kwa uchaguzi na kuondoka madarakani kwa Serikali iliyopo.

Nyingine ni kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, wafungwa wengine wa kisiasa na kuchukuliwa hatua kwa waliohusika na mauaji ya raia wakati wa vurugu za Oktoba 29 mwaka jana.

Hali ya Mkoa wa Tanga ulinzi ukiimarishwa wanachi wanaendelea na shughuli zao za kawaida.

Akizungumza jana jioni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alitoa hakikisho la usalama nchini na kuwataka wananchi wendelee kurejea katika shughuli zao.

Amesema hakuna huduma itakayositishwa na kwamba hakutatokea tena vurugu kama zilizowahi kutokea, akisema, “Never again.”

“Nawahakikishia, Serikali yenu iko salama, lakini vivyo hivyo nchi yenu iko salama. Serikali itaendelea kuwa karibu na wananchi na tunawaomba waendelee kutoa taarifa za kiusalama,” amesema.

Tumefikaje hapo

Akizungumzia mzizi wa tatizo, mwanahabari mkongwe, Absalom Kibanda, amedai uminyaji wa Watanzania kutoa maoni na uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha Taifa kufikia lilipo sasa.

Ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa wakati kukiwa na nguvu kubwa ya mitandao ya kijamii, hivyo watu wengi wanaamini chanzo cha habari kwa sasa ni majukwaa hayo.

“Binadamu tumeumbwa kupenda taarifa. Watu wanaona vyombo vya habari vinaminywa kwa njia ya kutishwa, kuvifungia na kiuchumi. Njia zote zinasababisha vyombo vya habari asilia kusinyaa na kukosa ubunifu.

“Kutokana na hali hiyo, mitandao ya kijamii inakuwa mbadala wa habari. Ombwe linazibwa na mitandao ya kijamii na wale wanahabari wa mtandaoni au mtaani. Lazima Serikali ikubali uhuru wa maoni, habari na vyombo vya habari ni muhimu katika hatua ya kidemokrasia,” ameeleza.

Mbali na hilo, Kibanda amesema kama kungekuwa na Bunge lenye wapinzani wengi, sehemu ya malalamiko ya wananchi yangepata nafasi ya kusikika katika mhimili huo.

“Leo CCM ina wabunge wengi bungeni. Matokeo yake kuna watu wengi wangekuwa bungeni leo, lakini kwa sasa wapo mtaani na mitandaoni wanakopeleka hasira zao kwa kificho na wazi,” amesema.

Amefafanua kuwa kurejesha uhuru, haki na wajibu katika maeneo ya demokrasia na siasa ni hatua muhimu ya kutoka katika hali iliyopo sasa.

“Hili suala linahitaji kutafakariwa, lakini tukirejesha uhuru, haki na wajibu katika maeneo hayo, yakiwemo pia ya demokrasia na siasa, ndiyo hatua ya kwanza kutoka hapa tulipo. Kwa nini kuna kilio kikubwa cha Katiba mpya sasa hivi? Kwa sababu kuna maeneo yameminywa,” amesema.

Tatizo halijatatuliwa

Kupitia picha mjongeo aliyoichapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Selemani Msindi, maarufu Afande Sele, amesema hofu na wasiwasi unaoendelea kujitokeza kila kunapotolewa wito wa maandamano unatokana na kutotatuliwa kwa sababu za msingi zinazochochea hali hiyo.

“Zile sababu zinazosababisha watu wafikirie kuandamana, hazijatatuliwa. Tunatumia nguvu kuzuia, lakini sababu zile hazijatatuliwa,” amesema na kuongeza kuwa njia pekee ya kukomesha hali hiyo ni kukubaliana kuangalia chanzo cha tatizo na kukitatua.

Ameeleza hata wanaotajwa kutolitakia mema Taifa wanaweza kutumia mazingira hayo kuleta shida nchini.

“Nafikiri ili mambo haya yaishe, ni kukaa chini tu, kurudi kwenye msingi wa tatizo ambao wote tunaujua. Vyama vyote vikae chini,” amesema.

Suluhu ya kudumu iko hapa…

Mchambuzi wa siasa, Profesa Baraka Mfinanga, amesema suluhu ya kudumu haiwezi kupatikana kwa maandalizi ya usalama pekee, bali kwa kushughulikia kiini kinachochochea  hali hiyo.

“Serikali, vyama vya siasa na wanaharakati wanapaswa kuwa na jukwaa la kudumu la mazungumzo. Kukosekana kwa mawasiliano kunafanya kila upande umtafsiri mwenzake kwa mashaka na tahadhari kubwa,” amesema.

Amesema mijadala kuhusu Katiba, haki za kisiasa na masuala mengine yenye mvutano inahitaji utaratibu rasmi unaokubalika na wadau wote, badala ya kusubiri migogoro inapojitokeza.

“Wananchi wanahitaji kuona kuwa kuna njia halali na zinazosikilizwa za kuwasilisha malalamiko yao. Imani hiyo inapokosekana, mvutano utaendelea kujirudia,” amesema.

Kujenga kuaminiana

Mchambuzi wa siasa, Dk Neema Kalinga, amesema msingi wa suluhu ni kuimarisha ushirikishwaji wa kisiasa na kujenga uaminifu kati ya taasisi na makundi yenye maoni tofauti.

“Kila upande ukihisi haujasikilizwa, matukio ya kuitana kwenye maandamano au kujiandaa kuyazuia yataendelea kujirudia. Msingi wa suluhu ni kurejesha imani ya pande zote.

“Nchi nyingi zimefanikiwa kupunguza migogoro ya kisiasa kwa kuweka ratiba za mazungumzo ya mara kwa mara, hata wakati hakuna mgogoro,” amesema.

Mazungumzo yatakayozingatia ukweli

Akizungumzia hilo, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema ni muhimu Serikali itekeleze pendekezo la Tume ya Uchunguzi wa Ghasia za Oktoba 29, lililotaka ikutane na wale wanaoonekana kutokubaliana na mwenendo wake.

“Kwa sababu tume iliundwa na Rais na imeshauri Serikali kwa jinsi walivyoliangalia jambo, nafikiri ilikuwa muhimu ushauri huo uzingatiwe. Watu wakae kwenye meza moja wajadili, kwa sababu njia ya mazungumzo ndiyo inayoleta ufumbuzi wa matatizo,” amesema.

Amesisitiza kuwa mazungumzo yatazaa matunda ikiwa ukweli utazingatiwa na pande zote.

Zisitumike nguvu

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Umoja wa Makanisa ya Dar es Salaam, Mchungaji Titus Kiame, amesema ni vyema Serikali ikawasikiliza wananchi badala ya kutegemea nguvu pekee za kiusalama.

Serikali inaweza kutatua

Mwanahabari Kibanda amesema watu wa kwanza wanaopaswa kuchukua hatua ni viongozi waliopo madarakani kwa sababu wana dhamana ya uongozi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema wanaochochea maandamano kutoka nje ya nchi wanapaswa kutafakari athari zinazowapata wananchi wa kawaida.

“Sisi wananchi wa kawaida ilikuwa mtu atoke akauze vitumbua au kufanya shughuli fulani. Sasa kama wateja hakuna barabarani, maana yake hawezi kufanya kitu. Maana yake ni uhujumu uchumi wa nchi yetu,” amesema.

Ametaka pia mchakato wa uchaguzi uheshimiwe na siasa zijengwe katika hoja badala ya kutumia wananchi kama ngao.

Ni hatari kwa mzunguko wa fedha

Mhadhiri wa Diplomasia ya Uchumi, Profesa Wetengere Kitojo, ametahadharisha kuwa hakuna anayetaka kuwekeza fedha zake katika eneo ambalo halina uhakika wa amani.

“Kelele zinazosemwa zinaweza zisiwe na ukweli wowote, lakini kutokana na historia ya Oktoba 29, shughuli lazima zisimame,” amesema.

Amesema kusimama kwa shughuli za uchumi, usafirishaji, kufungwa kwa benki na tishio la amani vinaathiri mzunguko wa fedha na Taifa linapoteza mapato.

Amesema haijalishi nini kinaendelea au yanadhibitiwa kwa kiwango gani, yote yanatuma ujumbe duniani kuwa Tanzania haina amani, hali inayoweza kutishia wawekezaji na wafanyabiashara.

“Pande zote zinazosuguana zikae mezani kumaliza tofauti zao ili hali ya maelewano irejee. Bila hivyo, haya yataendelea kuathiri nchi bila kujali yanatokea au yanadhibitiwa. Madhara yake ni makubwa hata kwa uvumi wake tu,” amesema.

Maelezo Serikali

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema mpango wa Serikali ni kudhibiti vitendo vyote vya uvunjifu wa amani nchini.

“Mpango kabambe ni kuhakikisha hakutokei matukio ya uvunjifu wa amani na kuwaondoa hofu wananchi ili akitokea anayeleta chokochoko apuuzwe na shughuli ziendelee kama kawaida,” amesema.

Msigwa amesema zaidi ya hapo wanaendelea kuwaelimisha wananchi kuwakataa wanaojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na kwamba hilo limefanikiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu (wa tatu kushoto) akiwa na wajumbe wa kamati ya usalama, wakiteta jambo na baadhi ya wananchi huku wakiburudika kwa kahawa kwenye kijiwe cha kahawa eneo la Manyema mjini Moshi baada ya kuzunguka maeneo mbalimbali ya mji huo kuangalia hali ya usalama leo Julai 7, 2026. (Picha na Mpiga Picha Wetu)

“Ukiangalia jana (juzi), pamoja na kwamba baadhi ya maeneo kweli biashara zilifungwa, lakini kuna maeneo mengi watu waliendelea na biashara hapa Dar es Salaam na hata mikoani,” amesema.

Amesema ni imani yake kuwa wanaofanya uhamasishaji wa matukio ya uvunjifu wa amani, itafika wakati watashindwa, kwani wameanza kupuuzwa.

Sambamba na hilo, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau, taasisi za kidini na viongozi wa kisiasa kuhakikisha wananchi wanapata elimu na wanaondokana na hofu.

“Hawa viongozi wa kidini tumekuwa tukizungumza nao na wale wa kisiasa. Tumekuwa tukijadili kuhusu umuhimu wa amani ya nchi yetu,” amesema.

Amesisitiza kuwa wapo watu wachache wanaochochea uvunjifu wa amani na wanaendelea kufuatiliwa kuhakikisha wanapatikana ili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *