
Dar es Salaam. Wakati uongezaji thamani mazao ya kilimo ikiwa ni moja ya mambo yanayopigiwa chapuo nchini, Chuo cha Ufundi Stadi na Mafunzo ya Ufundi (Veta) Mtwara kimekuja na mashine itayosaidia kuongeza zao la korosho.
Mbali na kubangua korosho hizo, pia mashine hiyo inaweza kutengeneza mvinyo kutoka kwenye mabibo ya korosho, jambo ambalo linaweza kumpa mkulima faida mara mbili.
Hili linafanyika wakati ambao kwa miaka mingi, mabibo ya korosho yamekuwa yakionekana kuwa sehemu isiyo na thamani kubwa na wakulima wengi wakuwa wakiyatumia kwa kiwango kidogo au kuyatupa.
Ubunifu huo unaonyeshwa katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) chini ya Nestory Agricola, unalenga kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya kutenganisha korosho na mabibo kisha kuyapatia matumizi ya kiuchumi.
Akiwa ni Mkufunzi wa Idara ya Uhandisi wa Mitambo na Umeme, Agricola amesema mashine hiyo ni toleo la pili baada ya kufanyiwa majaribio ya awali mwaka huu.
Amesema mbali na kutenganisha korosho na mabibo, mashine hiyo hukamua mabibo na kuzalisha juisi inayoweza kusindikwa zaidi kutengeneza bidhaa mbalimbali, ikiwemo mvinyo.
“Kupitia mashine hii tunaweza kuyakamua na kupata juisi ambayo inaweza kusindikwa zaidi na kuzalisha bidhaa nyingine za thamani,” amesema.
Amesema mashine hiyo imeundwa kwa kuzingatia mazingira ya wakulima wengi wa korosho, hasa walioko maeneo yasiyofikiwa na umeme.
“Hatukutaka kutegemea umeme kwa sababu mashamba mengi yako mbali na gridi ya taifa. Hivyo mashine hii inatumia injini ya petroli na inaweza kuvutwa kwa kutumia pikipiki au gari hadi shambani,” amesema.
Amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutenganisha hadi kilo 300 za korosho kwa saa kwa kutumia kati ya lita moja hadi mbili za petroli.
Amesema uwezo huo unasaidia kupunguza gharama ambazo wakulima walikuwa wanatumia kuajiri vibarua na muda mrefu wa kufanya kazi ya kutenganisha korosho na mabibo kwa mikono.
“Tunataka mkulima aongeze kipato si kwa kuuza korosho pekee, bali pia kwa kunufaika na mabibo ambayo awali yalikuwa hayatumiki ipasavyo,” amesema.
Agricola amesema wazo la kubuni mashine hiyo lilitokana na utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na mkufunzi mwenzake ambaye pia ni mkulima wa korosho, baada ya kushuhudia changamoto zinazowakabili wakulima.
Amesema malighafi zote zilizotumika kutengeneza mashine hiyo zinapatikana nchini, jambo linalorahisisha uzalishaji wake na kupunguza gharama za utengenezaji.
Hata hivyo, kwa sasa Veta Mtwara ina mashine hiyo moja pekee, lakini ipo katika mazungumzo na Bodi ya Korosho Tanzania ili kutathmini mahitaji ya soko na kuongeza uzalishaji.
“Pia tunatarajia kutengeneza toleo la tatu ambalo litakuwa na uwezo wa kutenganisha korosho na mabibo pekee kwa ajili ya wakulima wanaohitaji huduma hiyo bila kukamua juisi,” amesema.
Amesema mashine hiyo kwa sasa inauzwa kwa takribani Sh9 milioni, lakini bei inaweza kupungua kulingana na mahitaji ya mnunuzi na uwezo wa mashine utakaohitajika.
Amesema wakulima wanaweza kuinunua kwa ushirika ili kurahisisha upatikanaji wake kwa kuwa si kila mkulima ana uwezo wa kuigharamia peke yake.
Akizungumzia mashine hiyo, mmoja wa watembeleaji wa maonyesho hayo, Sabato Mapunda alitaka iangaliwe namna ya kutengeneza mashine zinazotumia umeme jua ili kupunguza gharama kwa wakulima.