Wanaharakati nchini Pakistan wameomba msaada wa mataifa mbalimbali kutokana na mzozo unaoendelea eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan na kusababisha serikali kuweka vizuizi vya kiuchumi ili kudhoofisha harakati za wananchi kudai haki zao.

Akizungumza na waandishi wa habari kiongozi wa asasi ya kiraia ya JAAC, Sardar Aman Khan inayoongoza madai hayo ya wakazi wa Kashmir amesema iwapo waandamanaji hawatasikilizwa, wataandamana kuelekea maeneo ya mipaka ya nchi hiyo kusaka msaada wa kibinadamu.

Maandamano hayo yameibuka siku chache baada ya wananchi kulalamika mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali, ankara kubwa za umeme na kuminywa kwa demokrasia.

‘’Waandamanaji na madereva wa malori tupo nao, hii leo wamesema vikosi vya usalama vya Pakistan vimeweka vizuizi barabarani kuzuia uingizaji wa unga wa ngano, chakula na mahitaji mengine muhimu. Hatua hii ni adhabu ya pamoja,” alisema Khan.

Alisema kutokana na vizuizi hivyo, maduka makubwa ya dawa katika miji ya Muzaffarabad na Rawalakot yameishiwa dawa muhimu na kusababisha wananchi kukosa  matibabu.

‘’Serikali imekata mawasiliano ya Intaneti na simu hatua inayodhoofisha biashara na shughuli za kila siku za kujitafutia riziki. Pia, gharama kubwa za umeme na mfumuko wa bei wa bidhaa zilizowekewa vikwazo zimefanya maisha ya wananchi kuwa magumu zaidi,’’ amedai Khan.

Hali hiyo imeibua mjadala katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ambapo wananchi wanahoji kinachoendelea na maisha yao ya kila siku.

Hadi sasa, ripoti za mashirika ya haki za kibinadamu ikiwemo Amnesty International zimedai kuna waliouawa katika maandamano hayo.

Hata hivyo, Serikali ya Pakistan inakanusha kuzuiwa kwa bidhaa muhimu na huduma za afya na kubainisha kuwa asasi ya JAAC inatumika  kuchochea vurugu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *