Tanga. Ukimkuta Dk Paul Msoka akiwa mbele ya darasa katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Kituo cha Tanga, huenda usitambue mara moja safari ndefu aliyopitia hadi kufikia hatua hiyo. Kwa utulivu na umahiri, anafundisha, anauliza maswali, anawasikiliza wanafunzi wake na kujenga hoja kwa kujiamini.

Kompyuta yake huzungumza, na simu yake husoma maandishi kwa sauti. Kupitia teknolojia hiyo, anaweza kuandaa mihadhara, kufanya tafiti na kuwasiliana na wanafunzi wake kwa ufanisi.

Lakini nyuma ya mhadhiri huyo mwenye Shahada ya Uzamivu kuna simulizi ya mtoto aliyepoteza uwezo wa kuona baada ya kumaliza darasa la saba; tukio ambalo wengi wangeliona kama mwisho wa ndoto zake za elimu.

Lakini kwake, tukio hilo lilikuwa mwanzo wa safari nyingine. “Nilipomaliza darasa la saba ndipo nilipopoteza uwezo wa kuona. Wazazi wangu hawakukata tamaa; walitafuta njia ya kuhakikisha ninaendelea na masomo,” anasimulia Dk Msoka katika mahojiano aliyofanya na Mwananchi jijini Tanga hivi karibuni.

Dk Msoka anasema alianza elimu yake ya msingi jijini Tanga akiwa na uwezo wa kuona bila tatizo lolote.

 Alisoma kama watoto wengine hadi alipohitimu darasa la saba.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, anasema maisha yake yalibadilika ghafla baada ya kupoteza uwezo wa kuona kutokana na madhara ya dawa aliyopewa alipokuwa akitibiwa malaria.

Anasema kupoteza uwezo wa kuona kulimlazimu kusitisha kwa muda ndoto yake ya kujiunga na sekondari. Badala yake, alitumia mwaka mmoja kujifunza maandishi ya Nukta Nundu (Braille), hatua iliyomfungulia tena mlango wa elimu.

Dk Msoka  anasema baada ya kumudu mfumo huo wa kusoma na kuandika, alijiunga na shule ya sekondari mkoani Shinyanga iliyokuwa ikitoa elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye ulemavu na wasio na ulemavu.

Anasema mazingira hayo yalimfundisha kuwa, uwezo wa mwanafunzi haupimwi kwa ulemavu alionao, bali kwa juhudi, nidhamu na dhamira ya kufanikiwa.

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, Dk Msoka anasema alijiunga na Chuo cha Ualimu Mpwapwa kusomea ualimu na alipohitimu, aliajiriwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga akiwa mwalimu.

Kwa wengi, kupata ajira kungekuwa mwisho wa safari ya elimu, lakini kwa Dk Msoka, ilikuwa hatua nyingine ya kuanza.

“Nilijua bado nina uwezo wa kusonga mbele. Sikutaka diploma iwe mwisho wa safari yangu ya elimu,” anasema.

Akiwa kazini, Dk Msoka alifanya mitihani ya kidato cha tano na sita kama mwanafunzi wa kujitegemea.

Anasema alifaulu na kupata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kusomea Shahada ya Kwanza ya Elimu.

Baada ya shahada ya kwanza, anasema aliendelea na Shahada ya Uzamili na baadaye Shahada ya Uzamivu (PhD), safari iliyomfikisha katika taaluma ya ualimu wa chuo kikuu, lakini njia hiyo haikuwa tambarare.

Dk Msoka anasema anakumbuka jinsi alivyokabiliwa na uhaba wa mashine za Braille, vitabu vya Nukta Nundu na teknolojia saidizi.

Anasema mara nyingi alitegemea watu wengine kumsomea vitabu ili aweze kuendelea na masomo.

“Tulikuwa na mashine chache na nyingi zilikuwa chakavu. Mara nyingi nililazimika kuomba watu wanisomee vitabu kwa sababu havikupatikana katika maandishi ya Braille,” anasema Dk Msoka.

Hata hivyo, anasema subira huvuta heri, kwa sababu mambo yalianza kubadilika alipofika chuo kikuu.

Anasema maendeleo ya teknolojia yalimpa uhuru aliousubiri kwa muda mrefu; kupitia programu zinazosoma maandishi kwa sauti, aliweza kusoma, kuandika, kufanya tafiti na kuandaa kazi zake bila kutegemea msaada wa watu wengine.

“Teknolojia imekuwa mkombozi wangu. Leo ninaweza kuandaa mihadhara, kufanya tafiti, kusoma vitabu vya mtandaoni na kuwasiliana na wanafunzi wangu bila kutegemea mtu mwingine,” anasema Dk Msoka.

Pamoja na changamoto za vifaa, Dk Msoka anasema alikutana pia na changamoto ya mtazamo wa watu. Anasema baadhi yao walimshauri afundishe katika shule za wanafunzi wasioona pekee, lakini hakukubaliana nao.

“Niliwaambia wanipeleke katika shule ya kawaida. Nilitaka kuthibitisha kuwa kinachofundisha si macho bali maarifa yaliyopo akilini mwa mwalimu.”

Anasema mwanzoni baadhi ya wanafunzi na walimu walikuwa na shaka kuhusu uwezo wake wa kufundisha.

Lakini kupitia mbinu shirikishi darasani, Dk Msoka anasema kwa kuuliza maswali na kusikiliza kwa makini majibu ya wanafunzi, kulimsaidia kujenga imani na kuthibitisha uwezo wake.

“Masikio yangu ndiyo macho yangu darasani. Kupitia ushiriki wa wanafunzi na majibu yao, ninaweza kujua kama wameelewa au la,” anasema daktari huyo wa taaluma.

Dk Msoka anasema mafanikio yake yanatokana pia na wazazi wake ambao hawakuwahi kuona ulemavu wake kama mwisho wa maisha.

Anasema jamii inapaswa kuwatambua watu wenye ulemavu kwa uwezo wao na mchango wanaoutoa badala ya hali zao.

“Sitaki nitambulike kwa sababu mimi ni mlemavu. Nataka nitambulike kwa kazi ninayoifanya na mchango ninaoutoa kwa jamii,” anasema Dk Msoka.

Kwa upande wa elimu jumuishi, anashauri Serikali na wadau kuongeza shule, walimu na vifaa vitakavyowawezesha watoto wenye uhitaji maalumu kupata elimu karibu na maeneo wanayoishi.

Kwa wazazi wa watoto wenye ulemavu, anasema: “Waamini watoto wao. Ulemavu si mwisho wa maisha. Elimu ndiyo silaha kubwa itakayowawezesha kuvuka vikwazo na kujenga maisha ya kujitegemea.”

Safari ya Dk Msoka inaonesha kuwa wakati mwingine giza linaweza kuwa mwanzo wa mwanga.

Kutoka mtoto aliyepoteza uwezo wa kuona baada ya darasa la saba hadi kuwa mhadhiri mwenye Shahada ya Uzamivu, ameandika simulizi ya maisha inayodhihirisha kwamba elimu, teknolojia, msaada wa familia na dhamira ya mtu binafsi vinaweza kubadili kabisa mwelekeo wa maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *