Timu ya taifa ya Norway imelazimika kuhama hoteli ya nyota tano jijini Miami, Marekani, baada ya kukaa usiku mmoja pekee, ikidai mazingira ya hoteli hiyo hayakuwa rafiki kwa maandalizi yao kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya England.

Norway, ambayo imefika hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia yake ya Kombe la Dunia, ilikuwa imefikia Hoteli ya The Dalmar iliyopo Fort Lauderdale.

Hata hivyo, viongozi wa timu hiyo waliamua kuhamia Hoteli ya Four Seasons iliyopo ufukweni baada ya kueleza kutoridhishwa na huduma na mazingira ya awali.

Miongoni mwa malalamiko yaliyotolewa ni uwepo wa shughuli za ujenzi karibu na hoteli, kukosekana kwa ukumbi wa mikutano wa timu, umbali wa takribani kilomita nne kufika ufukweni pamoja na madai ya baadhi ya wachezaji kutoridhishwa na kiwango cha usafi wa hoteli hiyo.

Hoteli ya The Dalmar iliyopo Fort Lauderdale, Miami ambayo Norway imehama kuelekea hoteli ya Four Seasons.

Nahodha wa Norway, Martin Ødegaard, amesema uamuzi wa kuhama umefanywa kwa lengo la kuhakikisha timu inapata mazingira bora zaidi kabla ya mchezo muhimu.

“Kulikuwa na mambo machache ambayo yangeweza kuwa bora zaidi, hivyo tukayarekebisha. Tulitaka kuhakikisha tunajiandaa kwa kiwango cha juu iwezekanavyo kwa ajili ya mchezo muhimu,” amesema Ødegaard.

Kocha wa Norway, Ståle Solbakken, amesema changamoto hizo hazikufanya hoteli ishindwe kukalika, lakini zilikuwa zinaathiri timu.

“Kulikuwa na mambo machache ambayo hayakuwa sawa. Tulihitaji sehemu ya kukutana kama timu na kufanya mikutano. Kulikuwa na mambo mengi madogo yaliyotulazimu kufanya uamuzi wa kuhama. FIFA imetuelewa na ikatusaidia kupata hoteli nyingine,” amesema Solbakken.

Meneja wa msafara wa Norway, Truls Daehli, amesema ingawa zoezi la kuhamisha timu nzima lilikuwa gumu, sasa wachezaji wote wanafurahia mazingira mapya.

“Tutakuwa hapa kwa takribani wiki moja na tunacheza mchezo mkubwa zaidi katika historia ya kizazi hiki cha timu. Tuliona ni muhimu kuweka hali nzuri na utulivu wa kikosi mbele. Kwa sasa kila mtu ameridhika,” amesema.

Muonekano wa hoteli ya Four Seasons iliyopo ufukweni ambayo Norway imehamia kutoka katika hotel ya The Dalmar. Picha na Mtandao

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Norway, gharama za hoteli mpya ni kubwa zaidi kuliko ile ya awali, ingawa FIFA ndiyo inayogharamia malazi ya timu zote zinazoshiriki mashindano hayo na inatarajiwa kurejesha fedha zilizotumika baada ya mchakato kukamilika.

Mbali na changamoto za malazi, Norway pia imekumbwa na tatizo la ugonjwa kambini. Kipa wa timu hiyo, Ørjan Nyland, amethibitisha kuwa baadhi ya wachezaji wameugua huku akisema daktari wa timu amekuwa na kazi kubwa ya kuwahudumia.

“Ni kweli tumekuwa na changamoto za kiafya. Tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila mchezaji anakuwa sawa kabla ya mchezo dhidi ya England,” amesema Nyland.

Katika wiki za hivi karibuni, Norway imelazimika kusafiri maelfu ya kilomita ndani ya Marekani ikihama kutoka Boston kwenda New Jersey, kurejea Boston, kisha Dallas na baadaye New Jersey kwa mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Brazil.

Vyombo vya habari vya Norway vinaeleza kuwa ratiba hiyo ya safari ndefu huenda imechangia uchovu na kuenea kwa maradhi ndani ya kikosi hicho.

Licha ya changamoto hizo, Norway itaingia uwanjani ikiwa na matumaini ya kuendeleza safari yake ya kihistoria kwa kuiondoa England na kutinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *