Mwanza. Watu 23 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa tuhuma za uchochezi, kupanga njama za kufanya vurugu na uhalifu mwingine katika maeneo wakati wa Sikukuu ya Sabasaba, Julai 7, 2026.

Miongoni mwa waliokamatwa ni shemasi wa Kanisa la EAGT, Philipo Chipuluko na Mwenyekiti wa Mtaa wa Ibungilo A, Wilaya ya Ilemela, Fantson Mpango.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa usiku jana Jumatano Julai 8, 2026 imeeleza kuwa, watuhumiwa hao walikamatwa kati ya Julai 5 na Julai 7, 2026 kupitia doria zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na hatua za kisheria zikikamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Waliokamatwa ni Mwalimu Deus Masalago (41), Mohamed Tosha (37) ambaye ni fundi ujenzi, Samwel Kobeli (38), Samwel Mtani (55), Fabian Nguvumali (52), Philipo Kulwa (37) na Fanuel Lutema (35) ambaye ni mwinjilisti.

Wengine ni Hamis Mwinyinuma (35), Julius Makonga (34), Philipo Chipuluko (38) ambaye ni Shemasi wa Kanisa la EAGT, Abdul Kagiwidi (27), Hassan Said (43), Alphaxad Nyamwafia (57), Abel Mwesa (62), Emmanuel Wambura (32) na Adamu Idd (23).
Wengine ni Philipo Maingu (31), Damas Sadoki (31), Edward Mikindo (28), Fantson Mpango (49) ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Ibungilo A, Wilaya ya Ilemela, David Mahendeka (31), Emmanuel Wangenyi (25) na Petro Mabula (40).

“Watuhumiwa hawa wamekamatwa kati ya Julai 5 na 7, 2026 kupitia doria zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza.

“Jeshi la Polisi linaendelea na taratibu za kisheria, ikiwamo mahojiano ya kina na taratibu zitakapokamilika, watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,” amesema Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa amesema hali ya usalama katika Jiji la Mwanza ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha doria za miguu na magari ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za watu wachache wenye nia ya kuvuruga amani, huku akisisitiza umuhimu wa kutii sheria za nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *