
Hayo yamo katika toleo la tatu la ripoti mpya ya Taswira ya Uwekezaji duniani wa Mali Zisizoshika kwa mwaka 2026 iliyotolewa huko Geneva, Uswisi hii Jumatano na shirika la Umoja wa Mataifa la Hakibunifu, WIPO kwa ushirikiano na Chuo cha Biashara cha Luiss kilichoko Roma, nchini Italia.
Uwekezaji katika ubunifu wazidi kuongezeka
Kwa mujibu wa ripoti hiyo:
- Uwekezaji katika mali zisizoshikika ulikua kwa wastani wa asilimia 5.5 kwa mwaka kati ya 2020 na 2025 ilihali uwekezaji katika mali zinazoshikika ulikua kwa asilimia 3.2 pekee kwa mwaka.
- Mali zisizoshikika sasa zinachangia karibu asilimia 13 ya pato la taifa (GDP) katika nchi 29 zilizofanyiwa utafiti.
- Ripoti imejumuisha kwa mara ya kwanza takwimu za Canada na Ufilipino pamoja na kusasisha taarifa za Brazil, India na Japan.
Mkurugenzi Mkuu wa WIPO, Daren Tang amesema tofauti hiyo inaonesha mabadiliko makubwa katika uchumi wa dunia. “Ongezeko hili la kihistoria la uwekezaji katika mali zisizoshikika linaonesha wazi kwamba thamani ya uchumi wa dunia inahama kutoka kwenye mali zinazoshikika kama vile mazao, madini, vifaa vya umeme, kwenda kwenye mali zisizoshikika. Takwimu hizi zinaonesha kuwa nchi na kampuni zinazidi kutegemea ubunifu, teknolojia na ubunifu wa kiakili kuendesha ukuaji wa uchumi.”
Amesema ni matumaini yake kuwa ripoti hii itawapa watunga sera uelewa wa mwenendo huu na kuwasaidia kuweka sera, mifumo na programu sahihi za kuwaunga mkono wavumbuzi na wabunifu.
Marekani bado inaongoza duniani
Ripoti inaonesha tofauti kubwa kati ya mataifa:
- Marekani iliwekeza karibu dola trilioni 5 katika mali zisizoshikika mwaka 2025.
- Japan imepanda hadi nafasi ya pili duniani kwa dola bilioni 810 mwaka 2024.
- Ujerumani inafuatia ikiwa na dola bilioni 695.
- Brazil iliwekeza dola bilioni 312 mwaka 2023.
- India na Ufilipino zimekuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kasi ya ukuaji wa uwekezaji katika mali zisizoshikika.
Akili mnemba(AI) yachochea wimbi jipya la uwekezaji
Ripoti inaeleza kuwa akili mnemba (AI) inachochea uwekezaji kupitia mawimbi mawili:
- Uwekezaji katika miundombinu ya kimwili kama vituo vya data, vifaa vya semikondakta, mifumo ya umeme na mitandao.
- Uwekezaji katika mali zisizoshikika kama data, programu za kompyuta, utafiti na maendeleo, chapa za biashara, mtaji wa maarifa ya taasisi na mafunzo ya wafanyakazi.
Ripoti inaongeza kuwa Marekani inaongoza katika mawimbi yote mawili, huku uwekezaji wake katika programu, data na mtaji wa maarifa ya taasisi ukiongezeka kwa asilimia 4.4 kati ya mwaka 2024 na 2025.
Kupima mali zisizoshikika ni muhimu
Ripoti hiyo inasisitiza kuwa mchango wa AI katika uchumi hauwezi kueleweka kikamilifu bila kupima vizuri uwekezaji katika mali zisizoshikika.
Cecilia Jona-Lasinio, Profesa katika Chuo cha Biashara cha Luiss amesema, “Akili mnemba si teknolojia mpya tu. Inabadilisha namna maarifa yanavyozalishwa, na kuufanya uwekezaji katika mali zisizoshikika kuwa msingi wa kuelewa athari zake za kiuchumi. AI hutegemea mali zisizoshikika kama data, programu na maarifa ya kitaasisi, na pia huzifanya kuwa na thamani zaidi kwa kupunguza gharama za kuzizalisha na kupanua matumizi yake.
Hata hivoy amesema, “sehemu kubwa ya uwekezaji huu, hususan katika mtaji wa maarifa ya taasisi, alama za biashara na mafunzo, bado hairekodiwi kikamilifu katika takwimu rasmi. Bila kuboresha namna mali hizi zinavyopimwa, tutaendelea kudharau mchango halisi wa AI katika uchumi na kukosa sera zinazoweza kunufaisha jamii kikamilifu”