
Klabu ya Sekhukhune ya Afrika Kusini, imetangaza kuwatema wachezaji wake watatu akiwemo straika mmoja wa zamani wa Yanga.
Sekhukhune ambayo sasa inafundishwa na kocha Cedric Kaze ikimchukua baada ya kuachana na Kaizer Chiefs, katika wachezaji watatu iliowatema yumo Andy Boyeli.
Boyeli msimu uliopita aliitumikia Yanga nusu msimu kwa mkopo akitokea Sekhukhune, kabla ya kurudishwa dirisha la Januari 2026 kutokana na mabingwa hao wa Tanzania kushindwa kukubaliana na kiwango chake.
Leo Julai 9, 2026, Sekhukhune imemtema Boyeli ikimpa ‘Thank you’ baada ya kudumu klabuni hapo kwa misimu miwili.
Mbali na Boyeli ambaye mpaka anaondoka Yanga aliifungia mabao mawili pekee, pia Sekhukhune imewatema Tresor Tshibwabwa huku Shaune Mogaila akiondoka kwa makubaliano maalum ya kuachana kwa pande mbili.
Kaze ameanza hesabu za kusuka kikosi kipya akitaka kutafutiwa wachezaji wenye ubora zaidi kuziba nafasi walizokuwa wakizitumikia watatu hao.
Kocha huyo raia wa Burundi, amepewa mkataba mgumu akitakiwa kuibakiza timu hiyo kwenye nafasi kumi za mwanzo kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Msimu wa 2025-2026, timu hiyo ilimaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 44 baada ya kucheza mechi 30.