Viongozi wa upinzani nchini Zimbabwe wameapa kupinga ndani na nje ya nchi marekebisho ya katiba yanayomruhusu Rais Emmerson Mnangagwa kuongeza muda wa utawala kwa miaka miwili na kufuta uchaguzi wa moja kwa moja wa rais.

Muungano mpya wa upinzani wa People’s Coalition umesema utapeleka shauri katika Mahakama ya Katiba na pia kuomba Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuingilia kati.
Serikali inasema mabadiliko hayo yataleta utulivu wa kisiasa, lakini wakosoaji wanayaeleza kuwa yanadhoofisha demokrasia na kuimarisha utawala wa chama tawala. Msimamo huo unatangazwa siku moja tu baada ya Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe kusaini marekebisho ya katiba yanayoongeza muda wake wa kusalia madarakani hadi mwaka 2030.

Marekebisho hayo yanaongeza muda wa uongozi wa Rais na Bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kuondoa mfumo wa uchaguzi wa moja kwa moja wa rais, huku yakiruhusu rais kuchaguliwa na bunge.

Bunge la Zimbabwe lilipitisha marekebisho hayo mwezi uliopita baada ya chama tawala cha Zimbabwe Zanu-pf kupata wingi wa kura wa theluthi mbili unaohitajika katika mabunge yote mawili.

Nick Mangwana Msemaji wa serikali ya Zimbabwe amesema kuwa

Imesainiwa, imethibitishwa na kukabidhiwa rasmi – sasa ni sheria.

Dalili za Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, kusalia madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili mwaka 2028 zilianza kujitokeza takribani miaka miwili iliyopita.

Mwaka jana chama cha Zanu-pf kilipitisha azimio la kufanya marekebisho ya katiba ili kuongeza muda wa mihula ya urais. Pendekezo hilo liliidhinishwa na Baraza la Mawaziri mwezi Februari mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *