Makumi ya mamilioni ya Wairani na waumini kutoka nchi mbalimbali duniani waligeuza shughuli ya mazishi ya Kiongozi aliyeuawa shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa ajili ya mazishi kote duniani.

Shughuli ya siku sita ya mazishi na kumuaga Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilifanyika katika miji mitano — Tehran, Qum, Najaf, Karbala, na Mash’had — na kushirikisha umati mkubwa watu waliokuwa na shauku kubwa ambao umevunja rekodi zote za awali za mahudhurio ya watu katika mazishi.

Shughuli hiyo ilijumuisha siku tatu za mazishi mjini Tehran, siku mbili za maombolezo ya hadhara katika Grand Mosalla na siku moja ya msafara mkuu wa umma wa mazishi, huku kila moja ya miji mingine ikiandaa siku kamili ya kutoa heshima kwa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Waombolezaji wengi walisafiri kati ya miji mbalimbali, wakizidisha kiwango cha ushiriki na kuunda wimbi endelevu la mazishi ya Kiongozi Muadhamu.

Makadirio rasmi, yaliyokusanywa kutoka vyanzo vingi huru vya uwanjani na data za Serikali, yanathibitisha kwamba kati ya watu milioni 41 na 43 wameshiriki katika tukio hilo la kihistoria.

Takwimu hizi zinatokana na mchanganyiko kamili wa data ikijumuisha rekodi za abiria wa usafiri wa umma kwenda na kurudi kwenye maeneo ya shughuli ya mazishi, mawimbi ya simu za mkononi yanayotumika katika maeneo muhimu kama vile njia za kuelekea Grand Mosalla na mikusanyiko ya watu, wastani wa muda wa mahudhurio ya mtu binafsi wa takriban saa mbili na nusu, hesabu za kina za msongamano wa watu kwenye njia za mikusanyiko ya Tehran, vipimo vya eneo halisi kutoka Msikiti wa Jamkaran hadi Haram tukufu ya Bibi Fatima Maasuma huko Qum, na njia za kutoka uwanja wa ndege hadi kwenye Haram ya Imam Ali bin Musa al Ridha huko Mashhad.

Bahari kubwa ya waombolezaji, ambao walikuwa wakikusanyika tangu asubuhi na mapema, ilifuatana na gari lililokuwa limebeba miili ya mashahidi, na kufanya mitaa ya Jiji la Mash’had kuwa mandhari adhimu na mazishi yasiyo na kifani.

Kiwango kikubwa cha mkusanyiko huo hiyo jana kilipita maelezo. Kuanzia wakati gari lililokuwa na mili ya Ayatullah Khamenei na watu wa familia yake lilipoingia Mtaa wa Imam Reza, lilikuwa limezungukwa kabisa na mawimbi ya waombolezaji waliokuwa wamesafiri kutoka kila kona ya Iran, wote wakiwa wameungana katika huzuni na majonzi iliyoandamana na azma na ukakamavu.

Nyuso za washiriki katika mazishi hayo zilizojaa machozi na kuandamana na kaulimbiu za maombolezo na kulaani Marekani na Israel zilitawala anga, na kuunda mazingira ambayo waangalizi wanayaeleza kama mojawapo ya maonyesho ya kustaajabisha ya umoja wa kitaifa katika historia ya karibuni duniani.

Serikali ya Iraq, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, imethibitisha kwamba idadi ya washiriki katika mazishi ya Ayatullah Ali Khameni katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala ilikuwa watu milioni 10.

Bila shaka takwimu hizi zinaakisi mazishi makubwa zaidi yaliyorekodiwa katika historia, ushuhuda wenye nguvu na wa milele wa upendo mkubwa na utiifu usioyumba wa watu wa Irani na Umma wa Kiislamu kwa Kiongozi wao aliyeuawa kishahidi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na wanafamilia yake waliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi mnamo Februari 28, lililofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya makazi ya kiongozi huyo mjini Tehran.

Miongoni mwa waliouawa shahidi katika hujuma hiyo ya kushtukiza ni pamoja na mke wa Kiongozi mpya Iran Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, binti wa Sayyid Khamenei, mkwe wa kiongozi marehemu na mjukuu wake aliyekuwa na umri wa miezi 14.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *