Gazeti la Times la London limeripoti kwamba Rabi Mkuu wa Mayahudi wa Uingereza, Sir Ephraim Mirvis, amelitaka Kanisa la Uingereza kukataa kujadili ripoti inayoelezea vita vya Israel huko Gaza kuwa ni “mauaji ya kimbari,” akidai kwamba kupitishwa hati hiyo kunaweza kuharibu uhusiano kati ya Wayahudi na Wakristo uliojengwa kwa miongo kadhaa.

Gazeti hilo limeeleza kwamba Mirvis, pamoja na viongozi mashuhuri katika jamii ya Wayahudi wa Uingereza, wametangaza upinzani wao dhidi ya mipango ya Sinodi Kuu ya Kanisa la Uingereza (the Church of England’s General Synod) ya kujadili hati yenye kichwa cha manenno: “Wakati wa Ukweli: Imani Wakati wa Mauaji ya Kimbari,” inayojulikana kama “Kairos II,” kwa madai kwamba, imetumia maneno kama vile “mauaji ya kimbari,” “ukoloni” na “ubaguzi wa rangi” ikizungumzia sera za Israel kuhusiana na Wapalestina.

Gazeti la Times limeeleza kwamba hati hiyo unakosoa vikali vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza,” ikisema kwamba vita vya sasa vinakuja katika muktadha wa muda mrefu wa “ubaguzi wa rangi, ukoloni wa walowezi na ukandamizaji wa kisiasa.”

Sinodi Kuu – chombo cha juu zaidi cha kutunga sheria cha Kanisa la Uingereza – imepanga kujadili suala la kujumuisha hati hiyo katika orodha ya mada zinazotumiwa na Kanisa katika juhudi zake za kuelewa hali halisi katika Mashariki ya Kati, na kura itafanyika wakati wa mikutano ya Sinodi itakaoanza leo Ijumaa katika mji wa York.

Kuhani na rabi wa Kiyahudi, Jonathan Roman, ametoa wito wa kutupiliwa mbali hati hiyo akidai kwamba utumiaji wa maneno kama hayo unaweza kusababisha mvutano mpya katika mahusiano kati ya taasisi za Kiyahudi na Kikristo nchini Uingereza.

Pendekezo lililowasilishwa kwa Sinodi, kulingana na Times, linajumuisha uungwaji mkono kwa Wakristo wa Palestina, kueleza masikitiko na huzuni kwa mauaji ya raia na msisitizo wa kupinga chuki dhidi ya Wayahudi na chuki dhidi ya Uislamu. Pia linatoa wito kwa Kanisa kushughulikia hati kadhaa zinazohusiana na mzozo wa Israel na Palestina ili kuongeza uelewa wake wa hali halisi katika maeneo ya Palestina.

Hati ya Kairos II inasema kwamba vita vya Israel huko Gaza ni mwendelezo wa “mradi wa Kizayuni unaolenga kudhibiti Palestina yote na kuwaondoa wakazi wake wa Palestina,” na inaielezea Israeli kama “mradi wa kikoloni unaotegemea ubaguzi wa rangi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *