DAR ES SALAAM: KATIKA jitihada za kuzuia uharibifu wa barabara na kuhakikisha zinapitika wakati wote, hususan kipindi cha mvua, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanzisha mpango wa Vikundi vya Jamii (Community Based Routine Maintenance) unaolenga kutunza na kuboresha zaidi ya kilomita 15,000 za barabara kupitia vikundi hivyo.
Akizungumza na Daily News Digital, Mratibu wa Mpango wa CBRM wa TARURA Makao Makuu, Mhandisi Richard Missa, amesema mpango huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Lengo lake ni kushirikisha wananchi katika shughuli za matengenezo ya kawaida ya barabara ili ziendelee kuwa katika hali nzuri na kupitika kwa urahisi hasa kipindi cha mvua.
Mhandisi Missa amesema hadi sasa vikundi 302 tayari vimenufaika na mpango huo, ambao umetekelezwa katika maeneo ya Pangani, Lushoto, Korogwe, Rufiji, Mkuranga, Mvomero na Kongwa.

Amefafanua kuwa vikundi hivyo vinahusika na kazi mbalimbali za matengenezo ya kawaida ya barabara, ikiwemo kukata nyasi kandokando ya barabara, kuzibua mifereji na makaravati, kuondoa uchafu barabarani pamoja na kufanya shughuli nyingine ndogondogo zinazosaidia kuboresha hali ya barabara na kuongeza ufanisi wa matumizi yake.
Aidha, amesema kila kikundi hupewa mkataba wa kufanya kazi kwa siku 100 kwa mwaka, utaratibu unaowawezesha wanachama kuendelea na shughuli nyingine za kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Mhandisi Missa, vikundi hivyo vinajumuisha makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo vijana, wazee, wanawake, wanaume na watu wenye ulemavu. Pia, wanachama wanatakiwa kuishi ndani ya umbali usiozidi kilomita tano kutoka barabara husika ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.