Utawala wa Kizayuni wa Israel umemzuia Mufti Mkuu wa Palestina kuingia katika uzio wa Msikiti wa al-Aqsa jijini Al Quds (Jerusalem) kwa muda wa wiki moja baada ya kumteka nyara, katika hatua nyingine inayolenga viongozi wa kidini wa Palestina.

Vikosi vya Israel vimemkamata Sheikh Muhammad Hussein siku ya Ijumaa, muda mfupi baada ya yeye kutoa khutba yake katika Msikiti wa al-Aqsa, kabla ya kumwachia akiwa na amri ya kuzuiliwa kuingia katika eneo la msikiti huo kwa wiki moja, huku kizuizi hicho kikitegemea kuongezwa tena.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Palestina,  Sheikh Hussein alikamatwa kutokana na maudhui ya khutba yake, ambapo aliomba dua kwa ajili ya Wapalestina waliouawa na Israel na kwa ajili ya kuachiliwa kwa wale wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.

Mapema mwezi huu, makachero wa utawala wa Israel walimhoji na kumwekea vikwazo Sheikh Ekrima Sabri, mhubiri wa muda mrefu wa al-Aqsa na Mufti Mkuu wa zamani wa al-Quds, jambo linaloendeleza mfululizo wa marufuku dhidi yake katika miaka ya hivi karibuni.

Hatua hizi zinakuja wakati Israel ikizidisha vikwazo dhidi ya maeneo matakatifu ya kidini ya Palestina tangu utawala huo ulipoanzisha mashambulizi yake ya kigaidi ya kigaidi na mauaji ya kimbari huko Gaza na kuua Wapalestina wasiopungua 73,000 na kujeruhi wengine zaidi ya 172,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Zaidi ya Wapalestina 1,100 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu katika kipindi hicho, wakiwemo angalau watoto 243, kutokana na kuongezeka kwa uvamizi wa kijeshi, ghasia za walowezi wa Kizayuni.

Mwezi Juni, shirika la Amnesty International lililaani vitendo vya Israel katika Ukingo wa Magharibi, na kusema ni wazi kuwa Wapalestina wanapitia kampeni ya maangamizi ya kimbari yanayotekelezwa na Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *