DAR ES SALAAM: MAADHIMISHO ya Siku ya Mazingira yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha wananchi, hususan vijana na wadau mbalimbali, kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira kupitia ubunifu, urejeleaji wa taka na matumizi endelevu ya rasilimali.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Richard Muyungi, amesema Serikali inaendelea kuipa kipaumbele ajenda ya uhifadhi wa mazingira kwa kuimarisha sera na mikakati inayolenga kulinda rasilimali za taifa sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Amesema matumizi ya nishati safi, usimamizi endelevu wa rasilimali na uhifadhi wa mazingira ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Immaculate Sware Semesi, amesema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kuwakutanisha vijana, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia na sekta binafsi ili kubadilishana uzoefu na kuonesha ubunifu unaochangia utunzaji wa mazingira.
Amesema kupitia Kijiji cha Mazingira kilichoanzishwa katika maonesho hayo, wananchi wameendelea kupata elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira, usimamizi wa taka, tathmini ya athari za mazingira pamoja na mbinu bora za kuendesha shughuli za kiuchumi zinazozingatia misingi ya uhifadhi wa mazingira.

“Mafanikio ya uhifadhi wa mazingira yanategemea ushiriki wa kila mmoja wetu. Serikali, sekta binafsi, vijana, taasisi za elimu na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kuhakikisha tunalinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Dk Semesi.
Ameongeza kuwa NEMC inaendelea kuhamasisha wawekezaji na waendelezaji wa miradi kuhakikisha wanafanya tathmini za athari za mazingira na kijamii kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao, hatua ambayo inalenga kulinda mazingira na ustawi wa wananchi.
Aidha, Dk Semesi amesisitiza umuhimu wa kutenganisha taka zinakozalishwa na kuimarisha shughuli za urejeleaji, akieleza kuwa taka zina thamani kubwa kiuchumi na zinaweza kuzalisha ajira, kuongeza kipato na kufungua fursa mpya za biashara kupitia uchumi wa kijani.
“Kwetu sisi NEMC, taka si tatizo bali ni fursa. Tukizisimamia vizuri zinaweza kuwa chanzo cha ajira, malighafi za viwandani na maendeleo ya uchumi endelevu,” amesema.
Pia amesema vijana wanaendelea kuwa sehemu muhimu ya suluhisho la changamoto za mazingira kupitia ubunifu katika urejeleaji wa taka, matumizi ya teknolojia za kijani na ujasiriamali unaozingatia mazingira.
Kwa mujibu wake, NEMC inalenga kuimarisha ushirikiano na vijana, wasanii pamoja na vyombo vya habari ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi.

Mbali na mijadala, maadhimisho hayo yalijumuisha maonesho na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu uzingatiaji wa sheria za mazingira, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, ukaguzi wa mazingira na huduma mbalimbali za kitaalamu zinazotolewa katika sekta ya mazingira.
Maafisa wa Serikali wameeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, jamii na wadau wa maendeleo utaendelea kuwa msingi muhimu wa kulinda urithi wa mazingira wa Tanzania, huku ukifungua fursa za kiuchumi na kuendeleza uchumi wa kijani kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.